Tanga. Katibu Mkuu wa National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa hatua ya kukiandikia barua Chama cha Mapinduzi (CCM) kijieleze kuhusu kauli zilizotolewa na mmoja wa viongozi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga leo Jumapili, Mei 24, 2026, Doyo ambaye aligombea urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, amesema hatua hiyo imeonesha wazi kuwa sheria inasimamiwa bila kuangalia ukubwa au ushawishi wa chama.
“Hatua hii imeongeza matumaini kwa wananchi na vyama vya siasa kuwa ofisi ya msajili haifanyi kazi kwa upendeleo, bali inaangalia nani amevunja sheria na kuchukua hatua stahiki,” amesema Doyo.
Amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanaharakati na wanasiasa waliodai kuwa sheria za vyama vya siasa zilikuwa zikitumika dhidi ya vyama vya upinzani pekee, lakini hatua ya sasa dhidi ya CCM imeondoa tafsiri hiyo.
“Watu wengi walikuwa wakiamini kuwa sheria zinatumika kwa upande mmoja, lakini sasa imeonekana wazi kuwa anayevunja sheria ndiye anayechukuliwa hatua bila kujali anatoka chama gani,” amesisitiza.
Doyo anawataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuacha kutoa kauli zinazoweza kuleta taharuki au kuvunja sheria, akisisitiza kuwa kila chama kina wajibu wa kulinda amani, utulivu na mshikamano wa Taifa.
Aidha, amesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inapaswa kuendelea kusimamia sheria kwa uthabiti bila kuogopa shinikizo la kisiasa kutoka kwa chama chochote.
“Kuna wanasiasa wanaodhani wako juu ya sheria na wanaweza kusema chochote. Lakini ni muhimu wakafahamu kuwa taasisi za kisheria zina wajibu wa kusimamia sheria kwa masilahi ya Taifa,” amesema.
Doyo amesema kushindwa kwa taasisi zinazosimamia sheria kutekeleza wajibu wake kwa wakati kunaweza kusababisha migogoro ya kisiasa na kuvuruga amani ya nchi.
Katika hatua nyingine, Doyo amesema hata vyama vya upinzani vilivyowahi kuandikiwa barua na Msajili wa Vyama vya Siasa, vilitoa maelezo yao kwa mujibu wa sheria, jambo ambalo linaonesha umuhimu wa kuheshimu mamlaka za kisheria nchini.
Akiwa na mtazamo kama huo, Mwenyekiti wa UDP Mkoa wa Tanga, Peter Muhina ameunga mkono uamuzi wa Msajili kuwachukukulia hatua wanasiasa wanaotoa maneno ya kisiasa yanayoweza kusababisha machafuko kwa jamii, akiwataka kufanya siasa zenye hekima na busara na zinazolenga kutatua changamoto za wananchi.
“Hata mimi nilivyosikia hatua zinazochukuliwa na Msajili dhidi ya vyama vya sisasa niliona ni jambo jema na linalofanywa kwa mujibu wa sheria,” anasema Muhina.
Kwa upande wake, Ramadhan Juma, mkazi wa Jiji la Tanga, amesema vyama vya siasa vikifanya shughuli za kisiasa kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa, wananchi watanufaika na mikutano ya kisiasa inayofanywa na vyama hivyo kwenye maeneo yao wakiamini hatua hiyo itapunguza maeneo yasiyokuwa na msingi kwenye majukwaa ya kisiasa.















