Lissu arudi tena mahakamani kesi ya rasilimali Chadema

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amerudi mahakamani kuomba kujumuishwa katika kesi ya madai ya mgawanyo wa rasilimali usio sawa ndani ya chama hicho baina ya Bara na Zanzibar. Hii ni mara ya pili kwa Lissu kufungua maombi hayo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, baada ya…

admin Avatar

by

4 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amerudi mahakamani kuomba kujumuishwa katika kesi ya madai ya mgawanyo wa rasilimali usio sawa ndani ya chama hicho baina ya Bara na Zanzibar.

Hii ni mara ya pili kwa Lissu kufungua maombi hayo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, baada ya Mahakama kumkatalia katika maombi yake ya awali, pamoja na mambo mengine ikisema kuwa hakuweza kuonesha maslahi ya karibu katika kesi hiyo.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu (marehemu kwa sasa).

‎Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Awali, Lissu alifungua shauri la maombi kwa jina lake binafsi, akiomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo kama mdaawa wa lazima akidai kuwa ana masilahi makubwa katika kesi hiyo kwa kuwa, ndiye mwenyekiti wa chama na kwamba uamuzi wowote utamuathiri.

Wajibu maombi katika shauri hilo walikuwa ni wadai katika kesi ya msingi yaani Said na wenzake (mjibu maombi wa kwanza mpaka wa tatu mtawalia) kwa upande mmoja.

Wengine walikuwa ni wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu Chadema (mjibu maombi wa nne na wa tano mtawalia) ambao ni wadaiwa katika kesi ya msingi.

Wadai katika kesi ya msingi walimwekea pingamizi la awali wakiiomba Mahakama iyatupilie mbali maombi hayo bila kuyasikiliza, kwa madai kuwa yalikuwa na kasoro za kisheria, lakini alishinda pingamizi hilo, hivyo akapata fursa ya kusikilizwa.

Hata hivyo, Mahakama hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake uliondaliwa na Jaji Hamidu Mwanga aliyekuwa akiisikiliza kesi ya msingi pamoja na maombi hayo, ilimkatalia rasmi Lissu kujumuishwa katika kesi hiyo.

Katika uamuzi huo uliosomwa Alhamisi Aprili 30, 2026 na Naibu Msajili Hussein Mushi, Jaji Mwanga amesema Lissu hakuonesha alikuwa na masilahi ya karibu kumwezesha kustahili kuunganishwa katika kesi hiyo kwa jina lake.

Jaji Mwanga alisema kuwa masilahi aliyojaribu kuyaonesha Lissu si ya moja kwa moja bali ni ya kiuwakilishi au kwa sababu ya nafasi ya ofisi anayoishikilia kwa sasa uenyekiti, huku akisema kuwa nafasi hiyo inaweza kushikiliwa na mtu yeyote wakati wowote.

Alisema kwa mazingira hayo hayawezi kuifanya Mahakama kutumia Amri ya 1 kanuni ya 10(2) ya Sheria ya Mashauri ya Madai (CPC), kuamuru aunganishwe katika kesi hiyo, hivyo akayatupilia mbali.

Siku chache baada ya uamuzi huo Lissu amefungua tena maombi hayo mara hii akitumia wadhifa wake, yaani mwenyekiti wa Chadema badala ya jina lake binafsi kama ilivyokuwa katika maombi ya awali.

Katika shauri hilo la maombi mchanganyiko namba 12194 la mwaka 2026, wajibu maombi ni walewale kama walivyokuwa katika shauri la awali lililokataliwa.

Tayari wadaawa wote (pande zote) yaani mwombaji, Lissu na wajibu maombi wameitwa mahakamani kesho kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo na maelekezo ya Mahakama.

Kwa mujibu wa hati ya taarifa ya Mahakama ya tarehe ya kutajwa kwa shauri hilo, limepangwa kusikilizwa na Jaji David Ngunyale aliyepangiwa kusikiliza kesi ya msingi, baada ya kuondolewa kwa Jaji Mwanga kwa maelekezo ya Mahakama ya Rufani.

“Mnafahamishwa kwamba shauri tajwa hapo juu limepangwa kutajwa Mei 25, 2026, saa 2:45 Asubuhi mbele ya Jaji Ngunyale,” inasomeka taarifa hiyo iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo ambayo Mwananchi limeona nakala yake kwenda kwa wajibu maombi wa kwanza mpaka wa tatu na kuongeza:

“Mnatakiwa kufika katika Mahakama hii bila kukosa na mnapaswa kuwasilisha siku hiyo nyaraka zote ambazo mnakusudia kuzitumia katika kuunga mkono kesi ya upande wenu.”

‎Katika kesi ya msingi, wadai wanadai kuwa  kumekuwa na  mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

‎Pia, wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo, wanaomba Mahakama hiyo itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.

Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa  ni kinyume cha sheria na ni batili.

Vilevile wanaomba Mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.

Kwa sasa kesi hiyo inasubiri kutolewa uamuzi wa pingamizi la wadaiwa kuhusiana na uhalali wake wanaodai kuwa ni batili kwa kuwa imekiuka mastakwa ya kisheria kwa kutokubainisha muda wa kuanza kwa madsi yao (mambo wanayoyalalamikia).

Jaji Ngunyale amepanga kutoa uamuzi huo Mei 28,2026, ambao ndio utatoa hatima ya uhai wa kesi hiyo.

Kama atakubaliana na pingamizi hilo basi kesi hiyo itaondolewa mahakamani hapo. Lakini kama Jaji Ngunyale atalitupilia mbali pingamizi basi kesi hiyo itaendelea kusikilizwa katika hatua zinazofuata.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports