Dar es Salaam. Sakata la mgomo wa madereva wa malori nchini ulioitishwa Julai 1, 2026 limechukua sura mpya baada ya madereva hao kukataa wito wa kushiriki kikao kilichoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani Juni 23 na 24, kwa lengo la kujadili na kutafuta ufumbuzi wa malalamiko yao.
Badala ya kuhudhuria kikao hicho, madereva hao wamemwomba Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kutoa tamko kuhusu hatua ambazo Serikali imechukua au inapanga kuchukua kushughulikia madai yao.
Wamedai iwapo tamko hilo halitatolewa, wataendelea na mpango wao wa mgomo kama walivyopanga.
Kabla ya wito wa sasa, madereva hao walipata barua ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Januari 17, 2026 kuwa wizara imepokea barua kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, ikiagiza wakutane kujadili kero zao na kupeleka mrejesho kabla ya Aprili.
Hata hivyo, madereva hao wamedai kuwa kikao hicho hakikufanyika na wameshangaa kuitwa sasa baada ya wao kutangaza mgomo.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Ijumaa, Juni 19, 2026, Mkondo alisema walipata barua ya kuhudhuria kikao cha Dodoma jana (Juni 19, 2026) kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kikao ambacho kinatarajiwa kufanyika Juni 23 na 24 kuanzia saa 3:00 asubuhi katika ofisi za wizara hiyo.
Hata hivyo, Mkondo amesema hawako tayari kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa maagizo yalielekeza kifanyike tangu Aprili mwaka huu, lakini watendaji hao wa Serikali waliwapuuza mpaka walipoona tangazo lao la kuitisha mgomo.
“Haya maagizo ya sisi kukaa kikao na Wizara ya Mambo ya Ndani yalitolewa na Waziri Mkuu kwa wizara hiyo baada ya kumfikishia malalamiko yetu Aprili mwaka huu.
“Maagizo yalikuwa kuundwa kwa kamati chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kikao chake kifanyike Aprili, ambacho pia kingehusisha wizara nyingine zinazohusiana na shughuli zetu.
“Hata hivyo, kwa sababu wanazozijua wasaidizi wake hao, hawakufanya hivyo, jambo ambalo tunalitafsiri ni dharau kwa kiongozi huyo mkubwa na kwetu pia madereva.
“Ndio maana hapa tulipofikia tunahitaji kumsikiliza Waziri Mkuu tu katika kushughulikia changamoto zetu na si hao watu wa Wizara ya Mambo ya Ndani au wizara nyingine, ambazo tulishaziandikia barua za malalamiko yetu bila kutujibu chochote hadi leo,” amesema katibu huyo.
Mratibu wa kikao hicho alitajwa kuwa ni Lissu Jingi, ambaye amedaiwa tangu wakati huo hajawahi hata kuwasiliana nao.
Mwananchi ilimtafuta Jingi Jumatatu majira ya saa 9:36, alijibu kwa kifupi kuwa yeye si msemaji wa wizara.
“Ndiyo madereva hao wamenitaja katika malalamiko yao, lakini mimi si mzungumzaji wa wizara, hivyo siwezi kulizungumzia,” alijibu kwa kifupi ofisa huyo.
Jitihada za kumpata Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi zilikwama baada ya simu yake kutopatikana hewani.
Taarifa ni kwamba, mbali na madereva, wengine watakaohudhuria kikao hicho ni watu kutoka Wizara ya Ujenzi, Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra).
Gazeti hili lilipowasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu malalamiko ya madereva hao kupitia Mkurugenzi wa Idara ya Bunge na Siasa, Raymond Kaseko, alikiri ofisi hiyo kuwahi kupokea malalamiko ya madereva na kuwa baadhi yake yanashughulikiwa na Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini.
“Ni kweli tumewahi kupokea barua ya malalamiko ya madereva hao, lakini tumeshaielekeza Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini iyashughulikie. Nadhani ungewatafuta, wanaweza kuwa na taarifa sahihi ya walipofikia,” alisema Kaseko.
Hata hivyo, Wizara ya Kazi ilipotafutwa kupitia Kamishna Msaidizi wa Kazi, Emmanuel Mweta, alisema hawajafikiwa na barua hiyo.
Pamoja na hilo, Mweta alisema kisheria wanaopaswa kutangaza mgomo ni vyama vya wafanyakazi dhidi ya mwajiri na si Serikali, hivyo alikishauri chama cha madereva kama kina malalamiko, kifike katika ofisi ya kazi.
“Chama kinachopaswa kutangaza mgomo ni kile kilichosajiliwa na kutambulika kama chama cha wafanyakazi na kiwe kimefuata taratibu zote. Kinyume na hapo, anayetangaza mgomo ni sawa na kutenda uhalifu.
“Hata hivyo, kama hicho chama ambacho tunajua ni cha hiari kwa usajili wake kinaona kuna malalamiko yanayoweza kushughulikiwa na wizara yetu, ni vema kikayaleta chenyewe kama kinaona vyama vya madereva vilivyopo haviwezi kuyafanyia kazi,” amesema Mweta.
Mgomo huo ulitangazwa na Chama cha Madereva kinachojiita ‘Mkombozi Drivers Africa Group’ wiki mbili zilizopita, huku Katibu wa chama hicho, Selemani Mkondo, akieleza kuwa asilimia 80 ya madereva wa malori wanauunga mkono.
Msimamo huo umekuja baada ya Juni 15 kufanyika vikao viwili katika maeneo tofauti vilivyohusisha madereva wa malori, kimoja kikifanyika katika ofisi za Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam na kingine Latra.
Katika kikao kilichofanyika Trafiki, walikutana madereva, viongozi wa vyama vya madereva na wale wa makundi yao ya WhatsApp.
Hata hivyo, wakati ajenda kubwa ilikuwa ni kuzungumzia suala la ushirikiano kati yao na jeshi hilo, inaelezwa pia suala la mgomo liligusiwa.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, William Mkonda, alikiri kukutana na madereva hao na kuwa baada ya majadiliano ya kina iliamuliwa viongozi wao wakashughulikie suala hilo.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (Tadwu), Ramadhan Ramadhan, aliyekuwa kwenye kikao hicho, amesema msimamo wa chama hicho ni kwamba hakuna mgomo kwa kuwa walioutangaza si chama cha madereva kinachotambuliwa kisheria.
Hata msemaji wa vyama vya wamiliki wa malori, Chuki Shabani, aliyehudhuria kikao kilichofanyika Latra, amesema madereva hao kama wana madai yoyote wafike katika ofisi za vyama hivyo, lakini hawajafanya hivyo badala yake wanalalamikia mitandaoni.
“Tulishawaita waje watueleze malalamiko yao hayo ili nasi tuyafikishe sehemu husika, lakini hawajafanya hivyo. Badala yake tunaona wanalalamikia mitandaoni. Katika hilo tunawezaje kuwasaidia?” amesema Shabani.
Katika malalamiko yao, madereva hao wametaja madai saba wanayotaka yashughulikiwe, ikiwamo kuongeza kiwango cha chini cha mshahara kutoka Sh350, 000 hadi Sh1 milioni kwa mwezi.
Pia wanataka masharti ya uhuishaji wa leseni yarahisishwe, huku madereva wenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15 wakitaka kuondolewa baadhi ya masharti wanayoyaona mzigo usio wa lazima.
Vilevile, wanapinga gharama za mafunzo ya leseni zinazofikia Sh375, 000, wakisema kiwango hicho ni kikubwa ukilinganisha na mishahara wanayopokea.
Dai jingine ni kwamba wanataka Bandari Kavu (ICD) zote zilizopo ndani ya Jiji la Dar es Salaam zihamishiwe Kwala, wakiamini hatua hiyo itapunguza msongamano wa magari unaoendelea kushuhudiwa jijini.
Mbali na hilo, wanataka Serikali iboreshe miundombinu ya barabara wanazodai kuwa chanzo kikubwa cha ajali zinazohusisha magari makubwa.
Sambamba na hayo yote, wanataka kuwepo kwa mfumo bora zaidi wa kusikiliza na kutatua changamoto za madereva kwa wakati.
Madereva hao wanakerwa pia na uwepo wa maofisa wa Latra barabarani, wakitaka mamlaka hiyo ieleze kuhusu msingi wa kisheria wa baadhi ya shughuli za ukaguzi wanazofanya barabarani badala ya Trafiki.

















