Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Patrobas Katambi akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Wakimbizi Duniani ambayo huadhimishwa tarehe 20 ya mwezi Juni kila mwaka.Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi,Sudi Mwakibasi na kulia Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani(UNHCR),Barbara Doste.Maadhimisho hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
CAP PIC 2
Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Sudi Mwakibasi akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Wakimbizi Duniani ambayo huadhimishwa tarehe 20 ya mwezi Juni kila mwaka.Maadhimisho hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
CAP PIC 3
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), Barbara Doste akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Wakimbizi Duniani ambayo huadhimishwa tarehe 20 ya mwezi Juni kila mwaka.Maadhimisho hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
…………
Na Mwandishi Wetu,DAR ES SALAAM
Serikali ya Tanzania imeahidi kuendelea kulinda,kusimamia na kutekeleza haki za binadamu ikiwemo haki za raia wa Tanzania na Wakimbizi kutoka nchi mbalimbali wanaohifadhiwa hapa nchini ambapo pia imesema itaendelea kusimamia Amani na Usalama ili madhira yanayotokea katika nchi nyingine yasitokee hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mheshimiwa Patrobas Katambi(MB) wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Tarehe 20 ya mwezi Juni,kila mwaka huku kauli mbiu ya mwaka huu ikisema “Hadi Kila Mtu awe Salama”
Waziri Katambi akizungumza mbele ya Wakimbizi wanaoishi jijini Dar es Salaam ambao waliwawakilisha wakimbizi wanaoishi katika maeneo mbalimbali nchini amesema nchi ya Tanzania inajifunza kwa yaliyotokea nchi jirani huku akitoa ahadi ya serikali ya kuwahudumia Wakimbizi.
“Ni agizo la Mheshimiwa Rais,Dkt.Samia,watu wote ambao ni ndugu zetu Wakimbizi waliohifadhiwa hapa tutawahudumia hata pale itakapohitajika rasilimali za nchi yetu tutazitumia,Rais wetu amekua anafanya hivyo wakati wote hata pale tulipokosa ufadhili na fedha za wadhamini,UNHCR aliendelea kutushika mkono lakini wapo wengine ambao hawakupata tuliwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili wapate waongeze nguvu lakini zilipokosekana kabisa Rais wetu hakusita kuweka mkono wake ili Wakimbizi muendelee kuishi kwa amani na utulivu,tunawapenda ndugu zetu,mmetupa uzoefu mmetupa mifano na uhalisia na sisi tunajifunza kutoka kwenu” amesema Waziri Katambi
“Mmeeleza sababu zilizopelekea kukosekana kwa Amani katika nchi zenu,zipo sababu ambazo pengine zinafanana na zenu ikiwemo rushwa,kujipatia fedha kwa manufaa binafsi,utakatishaji fedha,ukwepaji kodi na magendo yanayonufaisha wachache na kuumiza walio wengi,ubadhirifu,wizi wa mali za umma,kughushi na kufanya udanganyifu,uhalifu wa kiuchumi,makosa yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi,uhaini,uchochezi wa vurugu,vurugu za kisiasa,vyeo na mali,ubaguzi wa kidini,kikabila na ukanda,utapeli na dhulma kwa wananchi,unyanyasaji wa kijinsia.” aliongeza Waziri Katambi
Waziri Katambi amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Katiba ya Mwaka 1977 na marekebisho yake chini ya Uongozi wa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambae ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,Bunge na Mahakama wataendelea kusimamia haki za binadamu,utii wa sheria,maslahi ya wananchi wote wakiwepo Wakimbizi.








