Mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia, timu ya taifa ya Brazil maarufu kama Seleção, imepata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Haiti katika mechi ya pili ya Kundi C iliyochezwa kwenye Uwanja wa Philadelphia, Pennsylvania, Marekani.
Brazil ilikuwa ikisaka ushindi wake wa kwanza katika mashindano hayo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Morocco kwenye mechi ya ufunguzi.
Katika mchezo wa leo, Brazil ilitawala kipindi cha kwanza na kufunga mabao yote matatu ndani ya dakika 45 za mwanzo.
Mshambuliaji Matheus Cunha aliifungia timu hiyo mabao mawili, la kwanza dakika ya 23 na la pili dakika ya 36 akimalizia pasi nzuri ya Vinícius Júnior.
Dakika ya 45+3, kabla ya mapumziko, Vinícius Júnior aliifungia Brazil bao la tatu na la kwanza kwake katika mechi hiyo, akitumia vyema pasi ya Lucas Paquetá na kuipeleka timu yake mapumzikoni ikiwa mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili, Haiti iliingia kwa nidhamu kubwa ya kujilinda huku ikijaribu kufanya mashambulizi ya kushtukiza, lakini haikufanikiwa kupenya safu ya ulinzi ya Brazil. Hadi filimbi ya mwisho, mabao matatu ya kipindi cha kwanza yalitosha kuipa Brazil ushindi muhimu.
Kwa upande wa Haiti, huu ni mchezo wa pili mfululizo kupoteza katika Kundi C, baada ya kufungwa bao 1-0 na Scotland kwenye mechi ya kwanza.
Ushindi huo unaifanya Brazil kuongoza Kundi C kwa pointi nne, idadi inayolingana na Morocco walio nafasi ya pili. Scotland wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi tatu, huku Haiti ikibaki mkiani mwa kundi bila pointi yoyote.












