Kikosi Cha Wekundu wa Msimbazi Simba kimefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la CRDB kwa kuifunga Coastal Union mabao 4-0, katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa leo Juni 20, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Katika mechi hiyo nyota wa kikosi hicho Libasse Gueye aliifungia Simba bao la kwanza la dakika ya 19, baada ya kupokea pasi nzuri ya kiungo, Neo Maema na kupiga shuti lililomshinda kipa wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, Wilbol Maseke.
Dakika ya 55, Simba ikapata bao la pili lililofungwa na beki wa kushoto, Nickson Kibabage aliyemaliza mpira uliookolewa na kipa wa Coastal Union, Wilbol Maseke aliyekuwa anaokoa shuti lililopigwa na Gueye.
Wakati Coastal Union ikipambana kusawazisha mabao hayo, dakika ya 75 Simba ilipata bao la tatu lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Rushine De Reuck baada ya beki wa kikosi hicho, Anthony Mligo kufanyiwa madhambi akiwa eneo la hatari.
Dakika ya 79, Clatous Chama akaifungia Simba bao la nne lililotokana na mpira aliotengewa na mshambuliaji wa kikosi hicho, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ na kuihakikishia timu hiyo ushindi unaoipeleka katika fainali ya Kombe la CRDB.
Kwa sasa matumaini ya kikosi hicho ya kutwaa taji hilo ililolikosa kwa misimu minne mfululizo na kwenda kwa watani zao Yanga huenda ikatimia.














