Heche ataja mambo manne Ruvuma, aibua mjadala uchumi na rasilimali

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche ameitaja Ruvuma kuwa miongoni mwa mikoa yenye changamoto kubwa za kiuchumi licha ya kuwa na rasilimali nyingi, akisema hali ya sasa ni mbaya kiasi kwamba “ukoloni ungeonekana bora zaidi.” Heche ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Juni 20, 2026 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliolenga…

admin Avatar

by

5 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche ameitaja Ruvuma kuwa miongoni mwa mikoa yenye changamoto kubwa za kiuchumi licha ya kuwa na rasilimali nyingi, akisema hali ya sasa ni mbaya kiasi kwamba “ukoloni ungeonekana bora zaidi.”

Heche ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Juni 20, 2026 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliolenga kuendeleza operesheni ya Katiba Mpya pamoja na kampeni ya kumtaka huru Tundu Lissu.

Akiwahutubia wananchi wa Wilaya ya Songea, Heche amesema Mkoa wa Ruvuma una rasilimali nyingi zikiwemo makaa ya mawe, gesi na fursa katika sekta ya kilimo na viwanda, lakini wananchi wake bado wanaendelea kuwa maskini.

Heche amesema licha ya miaka 65 ya Uhuru, hali ya maisha kwa wananchi bado haijabadilika kwa kiwango kikubwa, akidai kuwa rasilimali za mkoa huo hazinufaishi wananchi wa kawaida.

“Ruvuma ina makaa ya mawe ambayo watoto wenu walipigania, lakini yanaondoka kwa malori na malori huku Songea ikibaki maskini bila maendeleo ya kutosha ya miundombinu kama barabara,” amesema Heche.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara leo Jumamosi Juni 20, 2026 Wilaya ya Songea.

Heche pia amezitaja changamoto nyingine anazodai zinakwamisha maendeleo kuwa ni mifumo ya vyama vya ushirika, sekta ya gesi, kiwanda cha mbolea, ajira kwa vijana pamoja na mzigo wa kodi unaowakumba bodaboda.

Amesema katika baadhi ya mikoa ya kusini, ikiwemo Lindi na Mtwara, ameshuhudia wakulima wakikosa haki yao kutokana na kile alichodai kuwa mianya ya ubadhirifu ndani ya vyama vya ushirika.

Heche amedai kuwa vyama vya ushirika vya mikoa ya kusini, akikinyooshea kidole Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Masasi, Mtwara na Nanyumbu (MAMCU), akikiita “kupe” ambacho badala ya kujikita kuwajengea uwezo wakulima, kinajenga nyumba za wageni zisizokuwa na ubora, hivyo ni ngumu kupiga hatua za maendeleo.

Amefafanua kuwa wakulima wanalima, wanandaa mashamba wenyewe, lakini wakati wa mavuno wanakumbana na ushuru na tozo mbalimbali, kisha mazao yao wanakabidhi kwenye vyama vya msingi na vya ushirika.

“Ukipeleka kwenye vyama vya msingi kila kilo moja, kuna gharama inaitwa ya usimamizi na uendeshaji wa vyama vya ushirika, kuna kitu mtunza ghala, mkaguzi, dhamana ya utunzaji wa mazao ghalani, usafirishaji, gharama za usimamizi wa mauzo, usimamizi wilayani.

“Gharama za vifungashio, maendeleo ya zao, gharama hizo zote anatakiwa kuzilipa mkulima. Chadema tutakomesha mambo haya, maana watu hawa wanawaona nyie kama hamna akili.”

Hata hivyo, madai hayo ya Heche yamejibiwa na Mwenyekiti wa MAMCU, Azam Julajula, ambaye amesema:

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, leo akisimikwa kuwa Chifu wa Wangoni wa Mkoa wa Ruvuma leo Jumamosi Juni 20, 2026.

“Unaposema mkulima ni nani? Mimi nina ekari zaidi ya 200, kama kuna tozo au ushuru hata mimi nalipa.

“Nilichokigundua hizi siasa si za maendeleo, bali ni za kuwatia watu jazba ili kuonekana wananyonywa. Sipendi sana kuingia huko, maana katika mikoa iliyotulia ni kusini. Wanachokifanya wao wanachukua jazba za huko wanazileta kusini,” amesema Julajula.

Amesema hakuna mkulima anayelazimishwa kuuza mazao yake katika vyama vya msingi, kwa sababu kuna masoko huria ya kuuza bidhaa hizo, akisema mfumo wa stakabadhi za ghala ni wa hiari na wakulima wenyewe wanakubaliana kujiunga.

“Unaposema mkulima ananyonywa, katika hali ya kawaida ni kweli? Huku nyuma wale raia wa kigeni waliokuja kununua kiholela na watu walilipwa fedha mkononi, je, wao walikuwa wapi?

“Hizi ni siasa za kizamani za kuwatia watu jazba. Leo hii pembejeo ninazozipata, ningekuwa naingia dukani mwenyewe nisingezipata. Leo wakulima wanapata pembejeo bure. Wao wamewahi kutoa elimu kuhusu vyama vya ushirika?” amesema Julajula.

Julajula amesema Heche anadai wakulima wa kusini wananyonywa, akihoji katika Mkoa wa Mara amewasaidiaje wakulima wa maeneo hayo.

Katika mkutano huo, Heche pia aligusia kauli ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Patrick Mwanulenge, aliyoitoa bungeni alipokuwa akichangia Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/2027, akishauri bodaboda kutozwa kodi.

“Nimeshangaa mbunge wa Mbeya Mjini kusema bodaboda na machinga si maskini na kutaka wachangie Sh1,000 kila siku kwa ajili ya kujenga barabara.

“Fikiria leo huyu bodaboda akinunua bodaboda anatozwa kodi, akinunua petroli ya kuweka kwenye chombo hicho kuna kodi ambayo inakatwa kwa kila lita moja anayonunua,” amesema.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Mwanulenge, akichangia mjadala wa bajeti bungeni juzi, alisema machinga na bodaboda si maskini.

“Kwa mfano, mimi pale Jimbo la Mbeya Mjini nina bodaboda wasiopungua 10,000. Wale watu tukiwajengea uwezo mzuri, wakawa wanajichangia wenyewe hata Sh1,000 kwa siku, maana yake unaongelea Sh10 milioni kwa siku.

“Sasa kama ni Sh10 milioni kwa siku, ukipiga mara mwezi, mara mwaka ni pesa nyingi,” alisema.

Pia, mbunge huyo alisema katika jimbo lake hilo anao machinga 317,000 na kueleza kuwa ameshazungumza nao ambapo wakichangia Sh1,000 unaongelea zaidi ya Sh300 milioni kwa siku.

“Sisi kama Serikali hebu tuyarasimishe yale makundi, tutengeneze mfumo. Wale watu wanaweza kujikusanyia fedha zao wenyewe, wakajikopesha wenyewe, wakajikatia bima za afya wenyewe. Sisi ni kutengeneza tu mazingira mazuri kama Serikali badala ya kuhangaika na fedha za halmashauri ambazo zinakusanya Sh2 bilioni kwa mwaka, ambazo ukizigawanya ni sawa na hakuna,” amesema.

Akizungumza na wananchi wa Masasi, Mnyika amewataka Watanzania kudai Katiba mpya sasa badala ya kusubiri hadi mwaka 2028 kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Othman Chande.

Mnyika amesema wakati wa kampeni Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi ndani ya siku 100 ataanzisha mchakato wa Katiba Mpya, lakini tangu aanze muhula wake wa pili Novemba 2025, hadi sasa hakuna kilichofanyika.

“Kwa sababu wao wanachelewa, Chadema kitaongoza Watanzania kutengeneza mchakato wa Katiba ya wananchi kuanzia sasa hadi kieleweke,” amesema Mnyika.

Juni 17, 2026, Mnyika alitangaza wajumbe 11 wanaounda kamati maalumu ya Kamati Kuu yenye lengo la kukwamua na kuendeleza mchakato wa kukusanya maoni ya upatikanaji wa Katiba Mpya kabla ya mwaka 2027 ili kuchochea ustawi wa wananchi.

Kamati hiyo iliyopewa hadidu za rejea nne na muda wa miezi mitatu kutekeleza jukumu hilo inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala, ambaye ni mwenyekiti, huku Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Deogratius Mahinyila, akiwa katibu wa kamati hiyo.

Wajumbe wengine ni Ali Ibrahim, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee (Bazecha), Suzan Lyimo, Ruth Moleli, Katibu Mkuu wa Bawacha, Pamela Maasay, Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa chama hicho, Gaston Garubindi, Zeud Mbano, Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Boniface Jacob (Boni Yai), na washauri wawili ambao si wanachama wa chama hicho, Wakili Mpale Mpoki na Wakili Jeremia Mtobesya.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports