Vyama vya siasa Tanga vyataka wakandarasi wabanwe

Tanga. Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa mkoani Tanga wameitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo chini ya viwango vinavyotakiwa, wakisema hatua hiyo itasaidia kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora. Wito huo umetolewa Juni 20, 2026 wakati wa maandalizi ya kuupokea Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa…

admin Avatar

by

3 minutes

Read Time

Tanga. Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa mkoani Tanga wameitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo chini ya viwango vinavyotakiwa, wakisema hatua hiyo itasaidia kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Wito huo umetolewa Juni 20, 2026 wakati wa maandalizi ya kuupokea Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kuingia mkoani Tanga Juni 21, ukitokea Wilaya ya Pangani baada ya kupitia wilaya za Kilindi na Handeni ambako miradi mbalimbali ya maendeleo imekaguliwa, kuzinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Tanga, Ramadhan Manyeko, amesema miradi inayobainika kuwa na kasoro wakati wa ukaguzi wa Mwenge wa Uhuru inapaswa kuwajibisha wahusika ili kudhibiti ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Hatutaki Mwenge wa Uhuru uwe unakuta miradi yenye kasoro kutokana na watu kushindwa kuwajibika. Hali hiyo husababisha hasara kwa Serikali na jamii inayotarajia kunufaika na huduma zinazotolewa kupitia miradi hiyo,” amesema Manyeko.

Aidha, amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru pamoja na mkesha utakaofanyika katika Viwanja vya Lamore, ambapo huduma mbalimbali za kijamii zitatolewa, ikiwemo upimaji wa virusi vya Ukimwi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CUF Mkoa wa Tanga na mbunge wa zamani wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbaruku amesema wakandarasi wanapaswa kutekeleza miradi kwa uadilifu na kuzingatia viwango vya kitaalamu kwa kuwa wao na familia zao ni wanufaika wa huduma zinazotolewa kupitia miradi hiyo.

“Kama ni shule, zahanati au jengo lolote la Serikali lilijengwa chini ya kiwango, wahusika na familia zao nao watatumia huduma hizo. Hivyo ni muhimu miradi ikajengwa kwa ubora unaostahili ili kuepusha hasara na gharama za marekebisho ya mara kwa mara,” amesema Mbaruku.

Ameongeza kuwa madiwani wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa kuwa wanafahamu vizuri mahitaji na mazingira ya maeneo yao kuliko kutegemea wataalamu pekee.

Akitoa mfano, amesema katika ukaguzi wa mradi mmoja wa Mwenge wa Uhuru uliofanyika mwaka jana eneo la Tongoni, ilibainika kuwa baadhi ya vifaa vilivyotumika havikulingana na mazingira ya eneo husika.

Akizungumzia maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, amesema Mwenge huo utaingia wilayani humo Juni 22, 2026 kupitia Kata ya Kirare na utakimbizwa umbali wa kilomita 58.9.

Amesema Mwenge wa Uhuru utakagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh3.6 bilioni.

“Mwaka huu wananchi watapata fursa kubwa zaidi ya kushiriki shughuli za Mwenge wa Uhuru, ambao umebeba kaulimbiu isemayo, ‘Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane Kuleta Maendeleo’,” amesema Kolimba.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, miradi itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru ni pamoja na zahanati ya Kirare, ofisi ya kata, kituo cha mafuta, kituo cha polisi, barabara, miradi ya vijana, nishati safi ya kupikia na miradi ya maji.

Amesema baada ya shughuli za Kirare, Mwenge utaelekea Kange kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa barabara, kisha Nguvumali kukagua miradi ya vijana, baadaye Shule ya Galanosi kwa ukaguzi wa mradi wa nishati safi kabla ya kuhitimisha mbio zake kwa mkesha katika Viwanja vya Lamore.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports