Asema mambo ya kutegemea wahisani yamepitwa na wakati
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kushirikiana na Serikali katika kutunza na kuhudumia vituo vya watoto wenye mahitaji maalumu na wasiojiweza badala ya kutegemea wahisani kutoka nje kwani mambo hayo yamepitwa na wakati.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Juni 21, 2026 katika harambee ya uchangiaji wa jengo la kitega uchumi cha kanisa la Anglika jijini Dodoma. “Mambo ya misaada yamepitwa na wakati na hata katika bajeti Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kusisitiza kuwa na bajeti ya nchi ambayo inategemea rasilimali za ndani ya nchi”.
Pia, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametoa rai halmashauri zote nchini ziandae orodha ya vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalumu na wasiojiweza na kuona namna ya kuvisaidia ambapo amesisitiza si vema kuwaandikia watu hao barua za kwenda kuomba misaada pindi wanapofika kwenye ofisi za umma.
Waziri Mkuu amesema awali katika maeneo mbalimbali nchini ilizoeleka kuwa vituo vya kulelea watoto yatima na wenye mahitaji maalumu viliendeshwa kupitia misaada kutoka nje ya nchi dhana ambayo watu wanatakiwa kuachana nayo.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahimiza Watanzania kuendelea kusimama katika mafundisho mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa dini ikiwemo kuendeleza amani na umoja wa kitaifa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan analipongeza Kanisa la Anglikana Tanzania kwa kuendeleza mradi wa ujenzi wa kitega uchumi kwa sababu ukuaji wa uchumi ni miongoni mwa malengo muhimu ya maendeleo.
Awali, Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Kasisi Canon Dkt. George Lawi alisema ili kuimarisha uwezo wa kifedha na kupunguza utegemezi, Kanisa la Anglikana Tanzania lilianzisha mradi wa kitega uchumi jijini Dodoma na kuhakikisha linakuwa na vyanzo endelevu vya mapato vitakavyowezesha utekelezaji wa majukumu ya kiroho na kijamii kwa ufanisi zaidi.
Alisema jengo hilo linatarajiwa kutoa huduma mbalimbali zikiwezo za hoteli, ofisi na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi wa kanisa na Taifa kwa ujumla. “Mradi huu umefikia hatua ya umaliziaji na umeshagharimu shilingi bilioni tatu na bado zinahitajika shilingi bilioni 1.5 ili kukamilisha na ndiyo sababu ya kufanya harambee leo.”
Pia, Dkt. Lawi alitumia fursa hiyo kumuahidi Waziri Mkuu kuwa Kanisa Anglikana Tanzania litaendelea kuwa mshirika wa Serikali katika juhudi za kuwaletea wananchi maendeleo endelevu kupitia sekta za elimu, afya, uwezeshaji wa jamii na kukuza maadili mema.
Katika harambee hiyo zaidi ya shilingi bilioni moja zilipatikana, ambapo pia Kanisa Anglikana limempa Heshima ya Kikanisa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Lay Canon, mshauri wa mambo ya Kanisa baada ya kuridhishwa na utendaji wake.














