Morogoro. Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kichangani kilichopo katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Sarah Ngonyani amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akidaiwa kuchangisha Sh2,000 kwa wananchi waliokuwa wakihitaji huduma ya uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa (Nida), huduma inayotolewa bure kwa mujibu wa utaratibu wa Serikali.
Akizungumza na Mwananchi leo Mei 24, 2026, Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Mvomero, Lukelo Bangu amesema taasisi hiyo ilianza uchunguzi baada ya kupokea taarifa za siri kutoka kwa wananchi waliodai kuwa baadhi ya watendaji wa vijiji walikuwa wakiwatoza fedha kati ya Sh2,000 na Sh5,000 kwa ajili ya kujaziwa fomu na kugongewa mihuri ya serikali ya kijiji ili wapate vitambulisho vya Nida.
Bangu amesema huduma hiyo hutolewa bure, lakini baadhi ya wananchi walilazimika kutoa fedha ili kuhudumiwa, hali iliyochochea malalamiko kwa Takukuru.
“Baada ya kupokea taarifa hizo, Mei 21, 2026, maofisa wetu walifika katika Kijiji cha Kichangani, Kata ya Mhonda kufanya uchunguzi na kuweka mtego wa kubaini ukweli wa tuhuma hizo na kumkata Ofisa Mtendaji wa Kijiji,” amesema Bangu.
Bangu amesema katika operesheni hiyo, Sarah Ngonyani alikamatwa akipokea Sh2,000 kutoka kwa mwananchi kama malipo ya kujaziwa fomu na kugongewa muhuri, jambo linalodaiwa kuwa kinyume cha utaratibu wa utoaji huduma.
Amesema mtego huo, pia, uliwezesha wananchi wengine kupata huduma bila kulazimika kutoa fedha huku uchunguzi ukiendelea kubaini ukubwa wa mtandao huo.
Diwani wa Kata ya Mhonda, Rashidi Juma amesema alipokea taarifa za kukamatwa kwa mtendaji huyo akiwa nje ya kata hiyo huku akidai kuwa katika mkoba wake zilikutwa noti tatu za Sh2,000, mojawapo ikiwa fedha ya mtego iliyotolewa na Takukuru kupitia mwananchi aliyeshirikiana na taasisi hiyo.
“Nafuatilia hili jambo kwa sababu nilikuwa safarini na taarifa nilizonazo ni kuwa alikutwa na Sh6,000 noti za Sh2,000 na moja ya noti ilikuwa ya hao Takukuru, huenda hiyo noti yao ndiyo imesababisha akamatwe,” amesema Rashid.















