Same. Serikali imetoa Sh44.1 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji wa Bwawa la Yongoma, unaotarajiwa kuwanufaisha wakulima zaidi ya 23,000 katika tarafa za Ndungu na Gonja, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha sekta ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao kupitia upatikanaji wa uhakika wa maji ya umwagiliaji kwa wakulima wa eneo hilo.
Akizungumza leo Mei 24, 2026 baada ya kutembelea eneo la mradi katika Kijiji cha Vumba, Kata ya Kagwiku, mkuu wa wilaya hiyo, Kasilda Mgeni ambaye aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, amesema kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa makubwa kwa wakulima wa tangawizi na mpunga wilayani humo.
Mgeni amesema mradi huo utakapokamilika utachochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Same kupitia ongezeko la uzalishaji wa mazao na mapato ya wakulima.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa wenye manufaa kwa wananchi wa wilaya hii, kwani mradi huu utakuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima,” amesema Mgeni.
Aidha, amewataka wananchi kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kulinda eneo linalotekekezwa mradi huo. Amesema Serikali itasimamia kwa karibu mradi huo na kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni akiwa ameambatana na Kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo kukagua eneo linalojengwa mradi wa umwagiliaji bwawa la Yongoma, kata ya Lugulu, wilayani humo.
Akizungumzia mradi huo, meneja wa mradi huo, Jacob Towa amesema mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wanachi 23,000 wilayani humo na unatarajiwa kukamilika mwaka 2029.
Amesema kwa sasa mradi huo umefikia asilimia nne na kwamba kukamilika kwake kutasaidia kuondoa changamoto ya ukosefu wa maji katika skimu za umwagiliaji za Ndungu, Kalemane, Vumba na Mpirani zinazohudumia wakulima 23,000.
“Ujenzi wa mradi huu ulianza Februari 2026 na tunatarajia kuukamilisha Februari 2029. Mradi huu utakapokamilika utawawezesha wakulima kulima zaidi ya msimu mmoja kwa mwaka, hali ambayo itaongeza uhakika wa upatikanaji wa mazao ya biashara kama tangawizi na mpunga kwa wingi, pamoja na mazao ya chakula,” amesema Towa.
John Gosso, mmoja wa wakulima wa tangawizi wilayani humo, amesema mradi huo utakapokamilika utawapunguzia changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo hasa katika kipindi cha kiangazi ikiwamo ya maji hupungua.
“Tunashukuru Serikali kwa kutuletea mradi huu mkubwa wa umwagiliaji hapa wilayani kwetu, wakulima sasa tutaondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya umwagiliaji wa mazao yetu,” amesema Gosso.
Mkulima mwingine wa tangawizi, Jerna Mdee ameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo ambao amesema utawanufaisha wananchi wengi ambao kwa vipindi tofauti wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya ukame na hivyo kusababisha mazao kukauka na hivyo wakulima kupata hasara.














