Hizi hapa fursa za diplomasia ya sanaa na utamaduni

Dar es Salaam. Serikali imesema Tanzania inaanza kunufaika na diplomasia ya sanaa na utamaduni huku matukio makubwa ya kimataifa yakitajwa kuwa lango jipya la fursa za kiuchumi, utalii na uwekezaji. Kauli hiyo imekuja wakati dunia ikizidi kuelekeza nguvu katika matumizi ya sanaa, michezo, lugha na utamaduni kama nyenzo za kuongeza ushawishi wa kimataifa, kukuza uchumi…

admin Avatar

by

3 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Serikali imesema Tanzania inaanza kunufaika na diplomasia ya sanaa na utamaduni huku matukio makubwa ya kimataifa yakitajwa kuwa lango jipya la fursa za kiuchumi, utalii na uwekezaji.

Kauli hiyo imekuja wakati dunia ikizidi kuelekeza nguvu katika matumizi ya sanaa, michezo, lugha na utamaduni kama nyenzo za kuongeza ushawishi wa kimataifa, kukuza uchumi wa ubunifu na kuimarisha ushirikiano wa maendeleo kati ya mataifa.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Majadiliano ya Tamaduni yaliyoandaliwa jioni ya Mei 24,2026 na raia wa China jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda alisema Tanzania imeanza kuona sekta ya utamaduni kama eneo jipya la fursa za kiuchumi na kijamii.

Alisema matukio ya kimataifa kama AFCON 2027 na Miss World 2027 si ya burudani pekee bali yanaweza kuwa majukwaa muhimu ya kuitangaza Tanzania duniani.

“Tanzania inaendelea kuona sanaa, michezo, lugha na utamaduni kama eneo jipya la fursa za kiuchumi na kijamii. AFCON 2027 na Miss World 2027 kufanyika nchini hapa si tu burudani bali ni majukwaa muhimu katika kutangaza utalii, uwekezaji na diplomasia ya utamaduni,” alisema Makonda.

Alisema kupitia matukio hayo, Tanzania inaweza kuvutia wawekezaji, watalii na kukuza biashara zinazohusiana na huduma, sanaa, mitindo, teknolojia ya ubunifu na utangazaji wa kimataifa.

Makonda alisema ushirikiano wa Tanzania na China katika sekta za utamaduni na sanaa umeendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa ubunifu na teknolojia, huku akiitaja China kama mshirika mkubwa wa maendeleo ya diplomasia ya utamaduni duniani.

“China imesimama na Afrika tangu enzi za mapambano dhidi ya ukoloni na imeendelea kuwa mdau muhimu katika ushirikiano wa maendeleo. Serikali inaamini matukio makubwa ya kimataifa yanaweza kutumika kuitangaza Tanzania duniani na kufungua fursa za uwekezaji, utalii na biashara,” alisema.

Katika maadhimisho hayo, viongozi wa Tanzania na China walisisitiza umuhimu wa kutumia mazungumzo ya tamaduni kama njia ya kujenga maelewano, amani na maendeleo ya pamoja duniani.

Siku ya Kimataifa ya Majadiliano ya Tamaduni ilipitishwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2024 baada ya kuungwa mkono na zaidi ya mataifa 80 duniani kufuatia pendekezo lililotolewa na Rais wa China, Xi Jinping, aliyesisitiza umuhimu wa mataifa kutumia tofauti za ustaarabu kujenga mshikamano wa dunia.

Kiswahili chabeba utamaduni wa Tanzania duniani

Mbali na sanaa na michezo, Makonda alisema lugha ya Kiswahili inaendelea kuwa nyenzo muhimu ya diplomasia na ushawishi wa Tanzania kimataifa kutokana na kuongezeka kwa matumizi yake katika mataifa mbalimbali duniani.

Alisema juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza Kiswahili kimataifa zimeendelea kuipa Tanzania nafasi kubwa katika diplomasia ya lugha na utamaduni.

Katika hafla hiyo, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian alisema mataifa mengi duniani yanaanza kutumia utamaduni, lugha na sanaa kama sehemu ya kuongeza ushawishi wa kimataifa na kuimarisha mahusiano ya kijamii na kiuchumi.

Aliitaja lugha za Kiswahili na Kichina kama chachu inayoeneza tamaduni za mataifa haya ulimwenguni huku ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili ukiendelea kuimarika.

“Ushirikiano wa Tanzania na China umeendelea kupanuka katika maeneo ya lugha, utalii, sanaa, ubunifu na miundombinu. Reli ya Tazara ni moja ya alama kubwa za ushirikiano wa kihistoria kati ya nchi hizi mbili,” alisema.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports