Mnyika: Mchakato Katiba mpya uanze 2026 si kusubiri 2028

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema chama hicho kinataka mchakato wa kupata Katiba mpya uanze mwaka huu 2026 na hakiko tayari kusubiri hadi mwaka 2028. Akizungumza katika muendelezo wa mikutano ya hadhara ya Operesheni ya Katiba Mpya na ‘Free Tundu Lissu’ iliyofanyika Dodoma, Mnyika amesema kupatikana…

admin Avatar

by

3 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema chama hicho kinataka mchakato wa kupata Katiba mpya uanze mwaka huu 2026 na hakiko tayari kusubiri hadi mwaka 2028.

Akizungumza katika muendelezo wa mikutano ya hadhara ya Operesheni ya Katiba Mpya na ‘Free Tundu Lissu’ iliyofanyika Dodoma, Mnyika amesema kupatikana kwa Katiba mpya wanaamini ndiyo njia ya kuhakikisha uwajibikaji, haki na ukweli katika kushughulikia matatizo sugu yanayowakabili Watanzania, ikiwamo hali ngumu ya uchumi.

“Ipo tiba kuu ya matatizo yanayolikabili Taifa kwa sasa, ikiwamo kuwa na Bunge dhaifu na urais wa kifalme. Tiba hiyo ni Katiba mpya ambayo tunataka mchakato wake uanza mwaka huu 2026, itakuwa suluhisho halisi la changamoto tunazopitia kama nchi,” amesema Mnyika.

Amesema hawakubaliani na ushauri wa ripoti ya Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande na mipango ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwamba wasubiri hadi mwaka 2028 na kuweka msimamo wapo tayari kuanza mchakato huo.

Mnyika amesema chama hicho kimejipanga kuzunguka nchi nzima kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa Katiba mpya, huku akieleza kuwa wanahitaji msaada wa rasilimali fedha na vifaa ili kufanikisha kampeni hiyo.

“Tuchangieni rasilimali fedha na vitu mbalimbali. Tunahitaji ujumbe wetu uwafikie wananchi wengi zaidi. Endapo mamlaka hazitachukua hatua na kuweka pamba masikioni, tumepanga kufanya maandamano nchi nzima kushinikiza madai yetu pamoja na kuachiwa huru kwa mwenyekiti wetu Tundu Lissu,” amesema Mnyika.

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Sharifa Suleiman amesema Tanzania ya sasa ina kizazi kinachohitaji haki huku akisema taifa linalotaka kupiga hatua za maendeleo haliwezi kukubali wananchi wake kutekwa.

“Licha ya Tanzania kuwa na mfumo wa vyama vingi, bado hakuna demokrasia ya kweli. Wananchi wanapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kupewa uhuru wa kutoa maoni yao,” amesema.

Amesema pia kuwa chama hicho kinapoizungumza ajenda ya Katiba mpya, lengo ni kupata viongozi wanaochaguliwa kwa njia halali ili waweze kuwajibika kwa maslahi mapana ya taifa pale yanapotokea matatizo au changamoto.

“Wananchi ni lazima mkiunge mkono Chadema kwa vitendo ili tuendelee kuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za Watanzania na kuhakikisha wanaishi kwa amani bila kunyanyaswa,” amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amesema vijana wa chama hicho si wa kufuata fikra za chama bila kutafakari, bali huchambua kwa kina masuala yanayotokea nchini na kutoa majibu yenye mantiki.

“Uhuru wa Tanzania ulipatikana ili kuwe na mazingira salama ya kuishi. Tunahitaji taasisi imara na mifumo inayozingatia maslahi ya wananchi, ndiyo maana Chadema tunaikumbatia ajenda ya Katiba Mpya,” amesema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mlezi wa Kanda ya Kati, Godbless Lema amesema kazi wanayoifanya ni ya kujitolea huku wakiweka rehani maisha yao kwa ajili ya kizazi kijacho.

“Ni heri binadamu akaishi miaka michache lakini akaacha alama ya kudumu, kuliko kuishi miaka mingi kwa kuogopa kifo na mwisho wa siku akafa bila mchango wowote wenye maana,” amesema.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, Dickson Matata amesema wananchi wanapaswa kulinda haki yao ya kuchagua viongozi wanaoweza kuwajibika katika kuboresha ustawi wao.

“Katiba mpya ndiyo suluhisho la mambo mengi. Tukiwa na msingi huo, itasaidia kulinda haki za wananchi, na viongozi watakaoshindwa kutekeleza wajibu wao watawajibishwa kupitia sanduku la kura,” amesema.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pemba, Omar Nassor amewataka wananchi kuikumbatia ajenda ya Katiba mpya, akisema itakapopatikana itasaidia kuimarisha amani na uhuru kwa wananchi wote.

“Chadema tunadai Katiba mpya kwa sababu iliyopo ina mapungufu mengi na haikidhi mahitaji ya Tanzania ya sasa. Kuendelea nayo kunaweza kuchochea kuvunjika kwa amani, kutowajibika na kudhoofika kwa umoja wa kitaifa,” amesema.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Boni yai amedai moja ya changamoto kubwa nchini ni kwamba watu wanaotetea haki wanateseka huku wahalifu wakitembea kwa uhuru.

“Chadema tunataka uwajibikaji. Haiwezekani mauaji ya raia wasio na hatia yafanyike halafu hadi sasa hakuna anayekamatwa wala kuhojiwa,” amesema Boniyai.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports