Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho ushindani wa ajira unaongezeka na teknolojia mpya kama akili unde zikibadili mfumo wa kazi duniani, wahitimu wa vyuo vikuu nchini wameonywa kutotegemea vyeti pekee kama tiketi ya mafanikio, bali kujenga uwezo wa ubunifu, maadili na kutatua changamoto za jamii.
Ujumbe huo umetolewa leo Mei 25,2026 na viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakati wa duru la kwanza la mahafali ya 56 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo wahitimu wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kuwa chachu ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika mahafali hayo, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema elimu ya juu inapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji kwa jamii.
Profesa Anangisye amesema, “Tumieni elimu mliyoipata kuleta faida kwa Watanzania na taifa letu. Elimu si mapambo ya mtu binafsi bali ni dhamana, wajibu na deni kwa taifa,”.
Akimnukuu Mwalimu Julius Nyerere, amesema viongozi wa taifa tangu enzi za uhuru walisisitiza kuwa waliofanikiwa kupata elimu wana wajibu wa kuitumia kuwahudumia wengine waliokosa fursa hiyo.
Profesa Anangisye amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika elimu, ujuzi na miundombinu ya vyuo vikuu ili kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Aidha, amesema wahitimu hawapaswi kukata tamaa endapo watachelewa kupata ajira rasmi kwa kuwa elimu waliyoipata inapaswa kuwa nyenzo ya kubuni fursa mpya kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ujasiriamali, kilimo, biashara, uchumi wa kidijitali na tafiti.
“Msikae mkisubiri ajira pekee. Elimu yenu iwasaidie kufikiri, kutatua changamoto na kuibua fursa mpya,” amesema.
Katika hatua nyingine, Profesa Anangisye amesema wahitimu wanapaswa kuwa mabalozi wazuri wa UDSM kwa kuzingatia nidhamu, uwajibikaji, uadilifu na moyo wa kulitumikia taifa.
Pia amesema matumizi ya teknolojia mpya, hususan akili unde, yanapaswa kuelekezwa katika kuleta manufaa kwa jamii badala ya kuharibu maadili na mshikamano wa kijamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Balozi Mwanaidi Maajar amesema dunia ya sasa inahitaji zaidi ya vyeti, kwani mafanikio yanategemea ubunifu, uwezo wa kuendana na mabadiliko na kutatua changamoto halisi za jamii.
“Jamii ya sasa haihitaji vyeti pekee bali inahitaji ubunifu, uadilifu na uwezo wa kutatua changamoto za watu. Mafanikio yenu yatapimwa kwa mchango mtakaoutoa katika kuboresha maisha ya jamii,” amesema Balozi Majar.
Amesema Tehama imekuwa nyenzo muhimu katika elimu, tafiti na utoaji wa huduma bora, hivyo wahitimu wanapaswa kutumia maarifa na teknolojia kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Balozi Majar amesema UDSM imewapa wahitimu si elimu pekee, bali pia maadili, ubunifu na maarifa ya kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi bora watakaochangia maendeleo endelevu ya Tanzania na dunia kwa ujumla.
Baadhi ya wahitimu waliozungumza na Mwananchi wamesema mafunzo waliyopata chuoni yatawasaidia kukabiliana na changamoto za soko la ajira na kutoa suluhisho katika jamii.
Mhitimu wa shahada ya uzamivu katika masuala ya elimu, Dk Neema Mushi amesema safari yake ya masomo ya juu imemjengea uwezo wa kufanya tafiti zitakazosaidia kuboresha sekta ya elimu nchini.
“Leo sihitimu kwa ajili yangu pekee, bali kwa ajili ya jamii inayohitaji maarifa na suluhisho. Nimejifunza kuwa msomi anatakiwa kuwa sehemu ya mabadiliko ya jamii,” amesema.
Kwa upande wake, mhitimu wa shahada ya uzamili katika Teknolojia ya Habari, Kelvin Mrema amesema kasi ya mabadiliko ya teknolojia inawataka vijana kuwa wabunifu badala ya kusubiri ajira za ofisini.
“Ujumbe wa viongozi wa chuo umetukumbusha kuwa teknolojia inaweza kuwa fursa kubwa kama tukitumia maarifa yetu vizuri. Vijana tunapaswa kubuni suluhisho za kidijitali zinazotatua matatizo ya Watanzania,” amesema.
Naye mhitimu wa shahada ya uzamili katika uchumi, Sophia Mgaya amesema changamoto ya ajira haiwezi kumalizwa kwa kusubiri kuajiriwa pekee, bali kwa vijana kutumia elimu yao kuanzisha miradi na biashara.
“Elimu ya sasa inatufundisha kufikiri tofauti. Tuna wajibu wa kutumia maarifa yetu kujiajiri na pia kuwasaidia wengine kupata fursa za kiuchumi,” amesema
Jumla ya wahitimu 878 wamehitimu katika ngazi mbalimbali za elimu huku asilimia 42.7 wakiwa wanawake.
Kati ya wahitimu hao, shahada ya uzamivu ni asilimia 9.4, shahada ya umahiri asilimia 60.6 huku wengine wakiwa katika ngazi za shahada ya awali na stashahada.















