Unguja. Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na athari za vita vya Mashariki ya Kati, hususan kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta kunakochangia ugumu wa maisha kwa wananchi.
Mbali na hilo, Dk Mwinyi amewasihi wananchi kudumisha umoja, mshikamano na upendo, akionya kuwa machafuko na migogoro huleta madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi.
Rais Mwinyi amesema hayo leo Mei 27, 2026 katika viwanja vya Tibirinzi, Pemba, wakati wa Baraza la Eid la Mkoa wa Kusini Pemba.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na viongozi wengine wa kitaifa wa dini na Serikali wakishiriki swala ya Eid iliyofanyika kitaifa leo Jumatano Me27, 2027 katika msikiti wa Ole Kianga Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba.
“Sisi sote ni mashahidi wa yanayoendelea katika nchi za Mashariki ya Kati ambazo zinaadhimisha sikukuu hii katika mazingira ya kukosa utulivu. Athari zake haziwaathiri wao pekee, bali dunia nzima ikiwemo Tanzania,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza athari zitokanazo na mgogoro huo wa vita, huku akiwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati juhudi za kukabiliana na changamoto hizo zikiendelea.
“Tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha nchi yetu inapunguza madhara yanayotokana na athari za migogoro hiyo. Nawaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kukabiliana na adha hiyo,” amesema.
Aidha, Dk Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano na kuondoa vitendo vya kubaguana au kudharauliana kutokana na tofauti za kijamii, akisema umoja ni msingi muhimu wa amani na maendeleo.
“Umoja na mshikamano wetu ni msingi muhimu wa kuwajali wengine katika jamii, wakiwemo wazee, masikini, wajane, yatima, wenye ulemavu na watu wenye changamoto mbalimbali. Tukifanya hivyo tutaendelea kuimarisha amani na ustawi wa nchi yetu,” amesema.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na viongozi wengine wa kitaifa wa dini na Serikali wakishiriki swala ya Eid iliyofanyika kitaifa leo Jumatano Me27, 2027 katika msikiti wa Ole Kianga Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba.
Katika hatua nyingine, ameahidi Serikali kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili mahujaji ili watu wengi zaidi wapate fursa ya kutekeleza ibada ya Hija, ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu.
Kwa mwaka huu, mahujaji 2,600 kutoka Zanzibar wamefanikiwa kwenda kutekeleza ibada hiyo nchini Saudi Arabia.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Sala na Mabaraza ya Eid Kitaifa, Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema kusikia na kutii ni msingi muhimu wa kudumisha umoja wa taifa na kuilinda nchi dhidi ya mifarakano.
Amewataka wananchi kuendelea kuwa wamoja, kushikamana na kuwa waaminifu kwa viongozi wao ili nchi iendelee kuwa na amani na maendeleo.
“Tujiepushe na fitina, uongo na chuki. Zanzibar ni ndogo, lakini wakati mwingine imejaa chuki, unafiki na uongo kutoka kwa baadhi ya watu. Hivyo ni muhimu kuwa wakweli na kushikamana kwa ajili ya maslahi ya taifa,” amesema.















