Idd ilivyobeba mambo manne | Mwananchi

Dar es Salaam. Hatua dhidi ya athari za kupanda kwa gharama za maisha, kudumishwa amani, mshikamano na maridhiano ni miongoni mwa mambo yaliyosikika zaidi kutoka katika mimbari za misikiti mbalimbali nchini, wakati wa swala ya Sikukuu ya Idd El Adh’haa. Mambo hayo yameelezwa na viongozi wa dini na Serikali walipokuwa katika ibada hiyo, inayowaunganisha Waislamu…

admin Avatar

by

8 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Hatua dhidi ya athari za kupanda kwa gharama za maisha, kudumishwa amani, mshikamano na maridhiano ni miongoni mwa mambo yaliyosikika zaidi kutoka katika mimbari za misikiti mbalimbali nchini, wakati wa swala ya Sikukuu ya Idd El Adh’haa.

Mambo hayo yameelezwa na viongozi wa dini na Serikali walipokuwa katika ibada hiyo, inayowaunganisha Waislamu kote duniani, kuadhimisha tukio la utayari wa Nabii Ibrahim kumtoa mwanawe Issihaka kama dhabihu kwa amri ya Mungu.

Katika sikukuu ya Idd El Adh’haa ambayo pia huadhimisha kilele cha Ibada ya Hijja, waumini wa dini ya Kiislamu huchinja wanyama kama ng’ombe, mbuzi au kondoo na kugawa kitoweo hicho kwa wasiojiweza na jamaa zao.

Hata hivyo, mambo hayo yaliyozungumzwa na viongozi hao wakati wa ibada, yanaakisi mijadala inayoendelea nchini, ikiwemo amani, mshikamano, haja ya maridhiano na hatua za kukabili kupanda kwa gharama za maisha.

Viongozi hao wa dini na Serikali wametoa kauli hizo katika misikiti na nyakati mbalimbali, leo Jumatano, Mei 27, 2026 walipotoa hotuba na nasaha zao, wakati wa swala ya Idd El Adh’haa.

Akiwa katika Viwanja vya Tibirizi Pemba visiwani Zanzibar, ilikoswaliwa Ibada ya Idd, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na athari za vita vya Mashariki ya Kati, hususan kupanda kwa bei ya mafuta, kunakochangia ugumu wa maisha.

“Sisi sote ni mashahidi wa yanayoendelea katika nchi za Mashariki ya Kati ambazo zinaadhimisha sikukuu hii katika mazingira ya kukosa utulivu. Athari zake haziwaathiri wao pekee, bali dunia nzima ikiwemo Tanzania,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza athari zitokanazo na mgogoro huo wa vita, huku akiwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati juhudi za kukabiliana na changamoto hizo zikiendelea.

“Tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha nchi yetu inapunguza madhara yanayotokana na athari za migogoro hiyo. Nawaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kukabiliana na adha hiyo,” amesema.

Aidha, Dk Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano na kuondoa vitendo vya kubaguana au kudharauliana kutokana na tofauti za kijamii, kwa kuwa umoja ni msingi muhimu wa amani na maendeleo.

“Umoja na mshikamano wetu ni msingi muhimu wa kuwajali wengine katika jamii, wakiwemo wazee, masikini, wajane, yatima, wenye ulemavu na watu wenye changamoto mbalimbali. Tukifanya hivyo tutaendelea kuimarisha amani na ustawi wa nchi yetu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi ameahidi Serikali kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili mahujaji ili watu wengi zaidi wapate fursa ya kutekeleza ibada ya Hija, ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu.

Kwa mwaka huu, mahujaji 2,600 kutoka Zanzibar wameenda kutekeleza ibada hiyo nchini Saudi Arabia.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Sala na Mabaraza ya Idd Kitaifa, Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema kusikia na kutii ni msingi muhimu wa kudumisha umoja wa taifa na kuilinda nchi dhidi ya mifarakano.

Amewataka wananchi kuendelea kuwa wamoja, kushikamana na kuwa waaminifu kwa viongozi wao, ili nchi iendelee kuwa na amani na maendeleo.

“Tujiepushe na fitina, uongo na chuki. Zanzibar ni ndogo, lakini wakati mwingine imejaa chuki, unafiki na uongo kutoka kwa baadhi ya watu. Hivyo ni muhimu kuwa wakweli na kushikamana kwa ajili ya maslahi ya taifa,” amesema.

Maridhiano, amani, mshikamano

Ujumbe kuhusu amani, ulitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, aliyewatakia Watanzania wote kheri ya sikukuu na kuwasihi washerehekee kwa amani.

“Tusherehekee kwa moyo wa amani na upendo, huku tukiwakumbuka ndugu zetu wenye uhitaji na kuendelea kudumisha utu na ukarimu katika jamii. Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema apokee dua na sadaka zetu na aendelee kulibariki Taifa letu, ameandika.

Suala la amani, mshikamano na maridhiano, limezungumzwa pia na Kadhi wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Mbalazi wakati wa swala hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Amesema wananchi na Watanzania wote wanapaswa kurejesha maridhiano, umoja na mshikamano. Wapo waliotofautiana kwa mali, maneno, siasa, vyeo na madaraka, akieleza kila mwenye nafasi anapaswa kumpatanisha anayemweza ili kurejesha undugu wa dini, ubinadamu na utaifa.

“Lazima tuwe pamoja, sadaka iliyo bora ni kupatanisha ndugu waliogombana, leo ni siku ya mapatano, maridhiano, kuwa pamoja na kuishi kama atakavyo Mungu, kupitia siku hii tunajifunza mengi,” amesema Dk Mbalazi.

Ameongeza kuwa, kwa sasa Watanzania wanapaswa kuendelea kuliombea Taifa juu ya amani ili iweze kupatikana haki na maendeleo, kwa kuwa wanapogombana wawili lazima kutuliza kwa kuuliza mkosaji.

“Kinachotangulia ni Amani, kisha haki kufuata, ndio maana hata Nabii Ibrahim alipouombea mji wa Makka, alitanguliza amani kisha akawaombea watu wa mji wake matunda, sisi tunaombea amani na maridhiano.

“Tunashukuru nchi yetu inaenda kwenye amani, tusipoteze jambo hili kwani itakuwa tatizo kwa vizazi vyetu, Mungu atusaidie katika hili ili tuweze kupata mafanikio na maendeleo,” amesema.

Akitoa salamu za Mkoa, Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya, Mohamed Aziz kwa niaba ya mkuu wa Mkoa huo, Beno Malisa, pia amewaomba wananchi kusherekea kwa amani, upendo na mshikamano.

“Lakini tusaidiane kwa mwenye nacho na asiye nacho kwa lengo la kujiwekea amana huko mbinguni, tujitokeze pia kujenga umoja wetu na kuchangia shughuli za dini haswa Uislamu,” amesema Aziz.

Katika hatua nyingine, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Omar, amesema sikukuu hiyo ni fursa ya kuendeleza upendo, mshikamano na amani miongoni mwa jamii.

“Hii ni sikukuu tukufu inayotukumbusha umuhimu wa ibada, upendo na mshikamano. Tunapaswa kusherehekea kwa amani na furaha,” amesema akiwa kwenye msikiti wa Mohamed VI, Kindononi.

Amesema siku hii si ya kuleta migogoro au vurugu bali ni ya kulinda amani na kuonyesha mshikamano wa kijamii.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kwenye msikiti huyo, amewatakia Waislamu na Watanzania wote sikukuu njema huku pia  akisisitiza umuhimu wa kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

“Ni muhimu kuendelea kuwa wanyenyekevu na kushirikiana bila kujali hali ya mtu, kwani taifa letu ni moja,” amesema.

Wakati huohuo, wanawake wa Kiislamu nchini, wametakiwa kuepuka kushindana kwa mavazi na mapambo yasiyo na tija, badala yake wazingatie maadili mema, hofu ya Mungu na malezi bora ya familia.

Akizungumza katika ibada hiyo iliyofanyika katika Msikiti wa Riadha mkoani Kilimanjaro, Sheikh Thabit Tarimo amesema wanawake wanapaswa kutambua kuwa uzuri wa kweli haupatikani katika mapambo ya nje pekee, bali katika tabia njema na ucha Mungu.

Amesema katika kipindi hiki wanawake wengi wamekuwa wakishindana katika mavazi na mapambo huku wakisahau misingi ya dini na maadili, inayopaswa kuwa kipaumbele katika maisha yao ya kila siku.

“Mnapenda sana kujipamba, lakini pambo lililo bora ni taqwa. Mnapenda kushindana kwenye mavazi, lakini nguo bora ni haya maadili mema,” amesema Sheikh Tarimo.

Amesema mwanamke mwenye maadili mema na anayemcha Mungu, ana mchango mkubwa katika kujenga familia imara na jamii yenye heshima.

Katika mawaidha hayo, Sheikh Tarimo pia amewataka wanaume kuhakikisha wanawahimiza wake zao pamoja na watoto kufanya ibada ya swala na kuzingatia mafundisho ya dini.

“Baba anaweza kuwa kila adhana inamkuta msikitini lakini mke wake haswali na watoto hawaswali, huku akiwa hafanyi juhudi yoyote ya kuwahimiza. Kila mmoja ataulizwa juu ya familia yake,” amesema.

Akiwa katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amewataka Watanzania, hasa wanaosafiri kwenda nchi jirani na wanaoishi katika maeneo ya mipakani, kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola katika kipindi cha sikukuu na hata baadaye.

Amesema Serikali imejipanga kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huo, huku wataalamu wa afya wakiwa wamewekwa katika mikoa ya mipakani ikiwemo Mara na Kigoma ili kuhakikisha usalama wa afya za wananchi unalindwa.

Kauli hiyo ya Mchengerwa, inajibu wito wa Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mohamed Said, aliyeiomba Serikali iendelee kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa Ebola.

Mchengerwa amewataka wananchi kuepuka mikusanyiko na kuchukua tahadhari zaidi katika kipindi cha sikukuu, akisisitiza Serikali ipo tayari kuchukua hatua za haraka pale dalili za ugonjwa zitakapoonekana.

“Aina ya Ebola inayozungumziwa sasa ni tofauti kwa sababu haina chanjo. Hivyo ni muhimu kwa wanaosafiri kwenda Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na maeneo ya mipakani na Kenya, Msumbiji na Zambia kuchukua tahadhari kubwa,” amesema Mchengerwa.

Amesema Mganga Mkuu wa Serikali na wataalamu wa afya wa mikoa mbalimbali wanaendelea kufanya kazi katika maeneo ya mipakani huku mikutano ya kimataifa ikiendelea Brazzaville kujadili namna ya kudhibiti ugonjwa huo.

Waziri huyo, amesema Ebola imejadiliwa na kutangwazwa katika Mkutano wa 79 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na kwamba kumekuwa na taarifa za kuongezeka kwa wagonjwa katika mataifa ya Uganda na DRC.

“Watanzania ni watu wa ushirikiano mkubwa, jambo ambalo linaweza kuongeza hatari ya maambukizi kama tahadhari hazitazingatiwa. Serikali imejipanga na ina vifaa pamoja na wataalamu wa kutosha kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini,” amesema.

Amesema mfumo wa maisha wa Watanzania wa kutembeleana na kushirikiana kijamii unaweza kuwa changamoto endapo ugonjwa huo utaingia nchini.

“Tumejengwa katika misingi ya ujamaa na ushirikiano iliyoasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere, lakini katika kipindi hiki ni lazima wananchi wawe waangalifu zaidi,” amesema.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amewahimiza wananchi wa mkoa huo kusherehekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu bila kujihusisha na vitendo vya fujo.

‎”Leo ni siku kubwa tumepewa na mwenyezi Mungu hakika ametubariki afya na itakuwa siku nzuri ya kupeana zawadi ya nyama baada ya kuchinja,” amesema.

Amewahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama wa kutosha katika kipindi chote cha sikukuu hiyo.

Imeandikwa na Tuzo Mapunda (Dar), Jesse Mikofu (Zanzibar), Saddam Sadick (Mbeya), Yesse Tunuka (Moshi) na Christina Joseph (Iringa)

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports