Dar es Salaam. Katika hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa mitaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya biashara nchini, Benki ya Absa Tanzania imezindua huduma mpya ya mikopo ya muda mfupi isiyo na dhamana, inayolenga kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kukuza shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi zaidi.
Huduma hiyo, inalenga wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya bidhaa na huduma, wakiwemo wauzaji wa jumla, wasambazaji, mawakala pamoja na wauzaji wa rejareja wanaotumia mifumo ya malipo ya kidijitali ya Absa, ikiwemo mashine za POS.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam jana Jumanne, Mei 26, 2026, Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa na Njia za Malipo wa Absa Bank Tanzania, Jane Kalumuna, amesema huduma hiyo inalenga kubadilisha mfumo wa jadi wa upatikanaji wa mikopo unaotegemea dhamana, na badala yake kutumia historia ya miamala ya biashara kama kigezo cha tathmini ya uwezo wa kukopa.
“Kwa muda mrefu, biashara nyingi zenye mtiririko mzuri wa fedha zimekuwa zikikosa huduma za kifedha kwa sababu hazina dhamana za kawaida. Kupitia Absa huduma hii, tunabadilisha simulizi hilo kwa kutambua na kuthamini utendaji halisi wa biashara,” amesema.
Mfumo huo utawawezesha wafanyabiashara kupata mikopo kwa haraka zaidi kulingana na mwenendo wa mauzo yao kupitia POS, hatua ambayo itaongeza mtaji na ufanisi wa biashara zao.
Kwa upande wake, Meneja Masoko, Mawasiliano na Chapa wa Absa Bank Tanzania, Beda Biswalo amesema huduma hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kuchochea ujumuishaji wa kifedha na kukuza uchumi wa taifa kupitia uwezeshaji wa sekta ya biashara ndogo na za kati.
Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa na Njia za Malipo wa Benki ya Absa Tanzania, Jane Kalumuna (wa tatu kushoto) na wengine kutoka kushoto; Meneja Masoko, Mawasiliano na Chapa, Beda Biswalo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na wa Kati, Scolastica Dominic na Meneja Mauzo wa Kitengo cha machine za malipo (POS), Edward Edwine, wakionesha mashine hizo kama ishara ya uzinduzi rasmi wa huduma ya mikopo isiyo na dhamana yenye lengo la kukuza biashara za wafanyabiashara wadogo na wa kati wanaofanya mauzo kwa kutumia POS za Absa.
“Kwa kuondoa kikwazo cha dhamana na kubadilisha mauzo ya kila siku kupitia POS kuwa chanzo cha haraka cha mtaji, tunabadilisha namna biashara zinavyopata huduma za kifedha nchini Tanzania. Tunaamini kuwa kila mfanyabiashara ana simulizi muhimu, na suluhisho hili linaakisi ahadi yetu ya kusikiliza na kusaidia ukuaji wao,” amesema Biswalo.
Kupitia huduma hiyo, benki inatekeleza dira yake ya kuwezesha ukuaji wa biashara barani Afrika kwa kurahisisha upatikanaji wa mtaji na kuimarisha uhusiano ya muda mrefu kati ya benki na wateja wake.
Hata hivyo, hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa mitaji inayowakabili wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, huku ikitarajiwa kuongeza kasi ya mzunguko wa fedha na kukuza ajira.
Huduma hiyo mpya inatajwa pia kuchangia kuimarisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali na kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara katika mfumo rasmi wa kifedha nchini.














