Dodoma. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa sasa hakina uongozi wa juu baada ya viongozi wake watatu kushikiliwa mahabusu kwa makosa ya uhujumu uchumi.
Waliokamatwa ni rais wa CWT, Seleman Ikomba, Katibu Mkuu, Joseph Misalaba na Mweka Hazina, Nashoni Kidudu ambao wameunganishwa na viongozi wastaafu Leah Ulaya ( aliyekuwa rais) na Japhet Maganga ambaye kabla ya uchaguzi wa mwaka jana alikuwa katibu mkuu.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na makosa 14 ya uhujumu uchumi, ikiwemo kujipatia zaidi Sh2.2 bilioni kinyume na sharia, kosa lililotendekea mwaka 2023 na 2024 wakati viongozi wa sasa walikuwa ni wasaidizi.
Kosa hilo linatokana na kuidhinisha matumizi ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa fulana na kofia kinyume na katiba ya CWT na shitaka hilo halina dhamana, hivyo watuhumiwa wataendelea kuwa mahabusu hadi shauri lao litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Uzoefu unaonyesha viongozi wakuu wa CWT waliowahi kufikishwa mahakamni huwa hawarudi kwenye nafasi zao na badala yake wanaokaimu ndiyo ambao hupanda.
Kwa sasa CWT italazimika kuongozwa na Shaban Ambindwile anayekaimu nafasi ya rais huku aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Protas Magesa akikaimu nafasi ya katibu mkuu. Nafasi ya mweka hazina inasubiri kikao cha kamati kuu.
Mei 25, 2026 viongozi hao wa CWT waliburutwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kwa makosa ya uhujumu uchumi.
Mmoja wa viongozi waaandamizi wa CWT ambaye amesema si msemaji, amesema katiba yao inatoa mwongozo huo kwamba kiongozi wa juu asipokuwepo, naibu au makamu wake anachukua majukumu ya moja kwa moja.
“Hilo haliwezi kusumbua, ingawa ni ukweli kutakuwa na shida kwa mweka hazina, maana katiba inataka kamati kuu iteue jina miongoni mwa wajumbe wake na ili kikao hicho kiitishwe zinatakiwa fedha na kwenye fedha kipengele ni kwamba lazima mweka hazina (ambaye hayupo) asaini,” amesema katibu huyo kutoka mmoja ya mikoa.
Amesema kwa namna hali ilivyo, itabidi wajumbe wakubali kujigharamia kwa haraka, ili waje kumteua mmojawapo na akithibitishwa, ndipo atasaini na oparesheni zingine za chama zitaendelea.
Hata kwa nafasi hiyo, amesema hakutakuwa na jambo geni kwani hata Nashon Kidudu (mweka hazina aliyeko ndani) aliingia kwa mtindo huo baada ya aliyekuwa akishikiria nafasi hiyo aliingia kwenye misukosuko.
Wawili hawa wanaingia kwenye tuhuma za uhujumu uchumi wakiwa wameweka rekodi ya kukataa nafasi ya uteuzi wa kuwa wakuu wa wilaya na wakataka waendelee kuwa na nyadhifa zao ndani ya CWT lakini aliyekuwa makamu wa rais, Dinna Masamani alikubali na kupelekwa wilaya ya Uvinza, Mkoa wa Kigoma.
Maganga pia aliingia kwenye msukosuko wa utoro kazini kutoka kwa mwajili wake, Manispaa ya Temeke, huku Ulaya akibwagwa kwenye kura na aliyekuwa makamu wake, Seleman Ikomba.
Kipindi cha uteuzi wa viongozi hao ndipo CWT ilipokuwa na migogoro ya ndani na ndipo aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Deus Seif alipofikishwa mahakamani kwa matumizi mabaya ya ofisi.
Mbali na Seif ambaye baadaye alikata rufaa na kushinda, pia aliyekuwa naibu katibu mkuu, Ezekiel Oluoch aliingia misukosuko na mwajiri na hata aliposhinda alizuiwa kurudi ofisini baada ya kuelezwa kiti kilishapata mwenyewe.














