MBEGU YA UCHUMI: Ugumu wa kukuza biashara ya kilimo kwa jembe la mkono

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na mabadiliko ya kushangaza katika maeneo mengi ya vijijini nchini, ambapo wakulima wanaacha kilimo cha mazao ya biashara na kuelekeza nguvu zao katika kuuza ardhi kwa ajili ya viwanja vya makazi. Mwelekeo huu unaibua mjadala mpana kati ya dhana ya kilimo cha kibiashara na kile kinachojulikana kama “hoe-culture” yaani…

admin Avatar

by

2 minutes

Read Time

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na mabadiliko ya kushangaza katika maeneo mengi ya vijijini nchini, ambapo wakulima wanaacha kilimo cha mazao ya biashara na kuelekeza nguvu zao katika kuuza ardhi kwa ajili ya viwanja vya makazi.

Mwelekeo huu unaibua mjadala mpana kati ya dhana ya kilimo cha kibiashara na kile kinachojulikana kama “hoe-culture” yaani kilimo cha jadi kinachotegemea jembe la mkono na mbinu zisizo na tija kubwa. Swali kubwa linalojitokeza ni kwa nini wakulima wanaacha mazao ya biashara na kukimbilia kuuza ardhi yao?

Kwanza, ni muhimu kuelewa kuwa kilimo biashara kinahitaji uwekezaji mkubwa, maarifa ya kisasa, na miundombinu imara. Wakulima wengi wadogo wanakosa mitaji, pembejeo bora, na masoko ya uhakika.

Hali hii inawafanya waone kilimo cha mazao ya biashara kama hatari kubwa, hasa wanapokumbwa na mabadiliko ya tabianchi, kushuka kwa bei za mazao, na gharama kubwa za uzalishaji. Kwa upande mwingine, kuuza kipande cha ardhi kwa ajili ya makazi huleta kipato cha haraka kisicho na hatari nyingi.

Pili, kasi ya ukuaji wa miji imeongeza mahitaji ya ardhi kwa ajili ya makazi. Maeneo yaliyokuwa mashamba sasa yanageuka kuwa vitongoji vipya. Wakulima wanapoona thamani ya ardhi ikipanda kwa kasi, wanashawishika kuuza badala ya kuendelea kulima. Kwao, ni fursa ya kipekee ya kupata fedha nyingi kwa wakati mfupi, jambo ambalo kilimo hakiwezi kulinganisha kwa urahisi.

Tatu, sera na mifumo ya usaidizi kwa wakulima bado haijawa rafiki vya kutosha kuhimiza kilimo biashara.

Ukosefu wa mikopo nafuu, bima za mazao, na huduma za ugani zinazofaa unachangia kudhoofisha ari ya wakulima kuwekeza katika kilimo cha kibiashara. Matokeo yake, wengi wanabaki katika “hoe-culture” yenye tija ndogo, au wanaamua kabisa kuachana na kilimo.

Hata hivyo, mwelekeo huu una madhara makubwa ya muda mrefu. Kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya biashara kunaweza kuathiri usalama wa chakula na mapato ya taifa.

Aidha, kupotea kwa ardhi ya kilimo kunapunguza uwezo wa vizazi vijavyo kujihusisha na uzalishaji wa chakula. Ni lazima tukubali kuwa kuuza ardhi ni suluhisho la muda mfupi, lakini linaweza kuleta matatizo makubwa baadaye.

Suluhisho liko katika kubadilisha kilimo cha jadi kuwa kilimo biashara yenye tija. Serikali na wadau wanapaswa kuwekeza katika miundombinu ya kilimo, kutoa mikopo nafuu, na kuimarisha masoko ya mazao.  Vilevile, elimu kwa wakulima kuhusu mbinu bora za uzalishaji na usimamizi wa biashara ni muhimu ili kuwafanya waone kilimo kama fursa ya kudumu ya kiuchumi.

Kwa kumalizia, uamuzi wa wakulima kuuza ardhi kwa ajili ya makazi si wa kubeza, kwani unatokana na mazingira halisi wanayokabiliana nayo. Hata hivyo, ni jukumu la pamoja kuhakikisha kuwa kilimo kinabaki kuwa mhimili mkuu wa uchumi.

Bila hatua za makusudi za kuimarisha kilimo biashara, tutashuhudia si tu kupungua kwa mazao ya biashara, bali pia kupotea kwa utambulisho wa jamii nyingi za wakulima. Wakati umefika wa kugeuza changamoto hii kuwa fursa ya mageuzi ya kilimo.

Makala hii imeandikwa na Dk Eliaza Mkuna

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports