Dar es Salaam. Ikiwa imepita miezi saba tangu alipojiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekia Wenje amesema hana mawasiliano yoyote na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Oktoba 13, 2025, Wenje alijiunga na CCM akitokea Chadema, ikiwa imepita miezi takribani tisa tangu uchaguzi wa ndani wa chama hicho ulipofanyika Januari 21, 2025 huku Wenje, aliyekuwa akigombea nafasi ya makamu mwenyekiti, akishindwa uchaguzi huo dhidi ya John Heche.
Wenje alikuwa akimuunga mkono mwenyekiti wa zamani wa Chadema, Freeman Mbowe, hata hivyo wote waliangushwa kwenye uchaguzi huo na Tundu Lissu akishinda uenyekiti pamoja na Heche aliyemuunga mkono.
Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Wenje, nyumbani kwake Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambapo amesema hana mawasiliano yoyote na viongozi wa chama chake cha zamani huku akisema kuwa upinzani haimaanishi usizungumze na walio CCM.
Hadi anaondoka Chadema, Wenye alikuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria na mjumbe wa kamati kuu ya Chadema. Amewahi pia kuwa mbunge kupitia chama hicho, hivyo alikuwa mmoja wa viongozi waandamini wa Chadema.
Wenje amebainisha kwamba mmoja wa viongozi waliokuwa watu wake wa karibu ni Heche, ambaye walikuwa zaidi ya wanasiasa, urafiki wao ulijengwa kwenye misukosuko ya siasa za upinzani, hawakuwa marafiki tu, bali ndugu, walishirikiana katika matukio ya kifamilia.
Kwa mujibu wa Wenje, tangu aondoke Chadema hajawahi kuzungumza na Heche wala viongozi wengine waandamizi akiwamo Boniface Jacob ‘Bon Yai’ na Godbless Lema, japo huzungumza na Joseph Mbilinyi (Sugu).
“Sugu amewahi kunipigia simu, actually siyo mara moja, yeye tunazungumza, ninachotaka kusema ni nini? Kuwa upinzani sio ndio kwamba hauzungumzi na viongozi wa CCM, wapo watu Chadema wana marafiki CCM na vivyo hivyo CCM wana marafiki Chadema,” amesema.
Katika hilo, Wenje ametolea mfano wa kaka yake Heche aliyemtaja kwa jina la Manchari, kwamba yeye yuko CCM na kwenye uchaguzi wa mwaka 2025 alishiriki kura za maoni kuwania ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Tarime Mjini na Ester Matiko.
“Ni ndugu yake na wanakaa meza moja na kula pamoja, lakini mmoja yupo CCM na mwingine Chadema, hivyo kuwa upinzani siyo uadui.
Wenje amesema: “Unafahamu kama Lissu aliwahi kugombea Singida kupitia TLP? Kaka yake, Alute (Mughwai) aliwahi kugombea kupitia CCM kura ya maoni na huyu Alute ndiye alimuondoa Lema kwenye ubunge, alikuwa wakili kwenye kesi yake baada ya Lema kushinda Arusha mjini mwaka 2010,” amesema.
Amesema katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM, Happy Kivuyo alifungua kesi kupinga matokeo, Alute Mughwai na Modest Akida ndiyo walikuwa mawakili wake, alishinda kesi hiyo na matokeo ya uchaguzi ule yakafutwa na kufanyika uchaguzi mdogo ambao Lema alishinda.
Katika mifano hiyo, Wenje amesisitiza kuwa upinzani sio uadui na masuala ya kisiasa hayapaswi kuchukuliwa katika mambo binafsi.
Wenje amesema hadi kuondoka Chadema ilikuwa ni uamuzi ambao alitumia muda kuufikiria, kutafakari hadi kuufanya, akibainisha kwamba katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu kuna majira na nyakati na ndivyo vilisababisha yeye ahame.
“Kama utakumbuka mambo mengi sana yalitokea kwenye uchaguzi wa ndani wa chama chetu (Chadema), tulimaliza uchaguzi Januari nikahamia CCM Oktoba, ilinichukua almost (takribani) miezi tisa.
“Muda nilioutumia hadi kuhama ulitosha kabisa kutafakari na kufanya uamuzi ambao naamini ni sahihi,” amesema.
Amesema nchini bado kuna changamoto ya ukomavu wa kisiasa kwa watu wengi na inapotokea kiongozi fulani anamuunga mkono fulani basi anaonekana ni adui, jambo ambalo si sawa.
“Kwenye chama cha Trump (Donald, Rais wa Marekani) wakati wa uchaguzi wapo watu wa chama chake hawakumuunga mkono na walieleza waziwazi kumuunga mkono Kamala Harris, lakini hawakufukuzwa.
“Hata Mwalimu Julius Nyerere (Baba wa Taifa), mwaka 1995, aliwahi kumuunga mkono mgombea ubunge wa NCCR Mageuzi pale Musoma Mjini, mbona chama chake hakikumfukuza?” amehoji Wenje.
Wenje amesema anaona ni kama chama chake cha zamani kimetengeneza wafuasi ambao wakiambiwa hiki kinapaswa kuwa hivi hata kama siyo sawa basi wataamini hivyo hivyo walivyoambiwa.
Amebainisha kwamba alipoamua kuhama hakumshirikisha mtu yeyote katika mipango hiyo ili kupata ushauri, akibainisha kuna mambo mengine yanapaswa kuchukua uamuzi binafsi.
“Kuna uamuzi mwingine ambao hushirikishi mtu, ukishirikisha wengine wanaweza kukushika mashati, hivyo mengine unafanya mwenyewe hata familia yako huwa huiambii,” amesema.
Amesema akiwa Chadema, waliishi kama familia lakini kuna makosa viongozi wengi huwa wanayafanya hasa pale mtu anapoamua kuchukulia binafsi masuala ya kisiasa.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Wenje amesema alikabiliana na tukio ambalo lilibadilisha maisha yake na kumfanya aishi maisha ya ukimbizi ambayo hakuwahi kuwaza kuyaishi.
Amesema Oktoba 30, 2020, ikiwa ni siku mbili baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, akiwa nyumbani kwake Kijiji cha Michire kilichopo Wilaya ya Rorya mkoani Mara, zilizuka vurugu ambazo hadi leo hazijafutika kwenye kumbukumbu zake.
Amesema siku hiyo alikuwa ameandaa sherehe ndogo ya kuwaaga watu waliokuwa pamoja naye kwenye kampeni baada ya uchaguzi kumalizika, wakati muziki ukiendelea, watu wa kijijini kwake wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya chakula na mazungumzo ya kawaida, polisi walitanda nyumbani kwake.
“Yalizuka madai kwamba kulikuwa na mipango ya maandamano, tulipigwa vibaya hali iliyosababisha taharuki kijijini, wazee wa kijijini hadi mama yangu walijikuta katikati ya vurugu hizo bila kutarajia, ilikuwa ni tukio kubwa.
Wenje amesema taharuki hiyo baadaye iligeuka kuwa kubwa zaidi kiasi cha kuathiri hata familia yake baada ya kaka yake kuuawa katika mazingira ya sintofahamu hiyo na tukio hilo ndilo lilisababisha yeye akaishi maisha ya ukimbizi nje ya nchi, maisha ambayo ni ya upweke na hayaelezeki.
“Sikuwahi kuyaishi maisha yale, ni mabaya, tusione tu kuna watu wanahamasisha vurugu, lakini ikitokea usiombe ikakukuta, hayo ni maisha magumu na mabaya, hayafai, tuendelee kuilinda tunu ya amani tuliyo nayo,” amesema.















