Baba Levo, Nondo kutunishiana misuli mahakamani

Dar es Salaam. Mvutano kati ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando (Baba Levo) na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, umechukua sura mpya baada ya kila upande kuonyesha dhamira ya kumfikisha mwenzake mahakamani kwa madai ya kuchafuliana taswira na kuharibu heshima zao. Chanzo cha mgogoro huo ni tuhuma ambazo kila mmoja…

admin Avatar

by

3 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Mvutano kati ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando (Baba Levo) na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, umechukua sura mpya baada ya kila upande kuonyesha dhamira ya kumfikisha mwenzake mahakamani kwa madai ya kuchafuliana taswira na kuharibu heshima zao.

Chanzo cha mgogoro huo ni tuhuma ambazo kila mmoja amekuwa akimwelekezea mwenzake. Wote wanadai kauli zinazotolewa dhidi yao zimekuwa zikidhalilisha na kuathiri sifa zao mbele ya jamii, hivyo wanataka madai hayo yathibitishwe kupitia vyombo vya sheria.

Baba Levo, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), anadai Nondo amekuwa akitoa kauli zinazopinga uhalali wa ushindi wake katika uchaguzi  Mkuu wa mwaka 2025, akidai ubunge wake ‘alijipachika.’ Kwa mujibu wa mbunge huyo, kauli hizo zinaharibu sifa yake na kupunguza imani ya wananchi aliowawakilisha.

Kwa upande wake, Nondo anamtuhumu Baba Levo kwa kusambaza taarifa anazodai ni za uongo dhidi yake, ikiwemo madai kwamba aliwahi kujiteka mwenyewe. Nondo anasisitiza kuwa Mahakama ilishamtakasa dhidi ya tuhuma hizo, hivyo anaona kauli hizo ni za kumchafua na kumdhalilisha.

Awali, kila upande ulimpa mwenzake siku saba za kuomba msamaha hadharani. Hata hivyo, hakuna aliyetekeleza matakwa hayo, jambo lililoifanya pande zote mbili kuonyesha utayari wa kutumia njia za kisheria kutafuta haki na kulinda heshima zao.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Mei 31, 2026, Nondo amesema haoni sababu ya kuomba msamaha kwa madai aliyoyatoa, akieleza Baba Levo hajawahi kumfuata rasmi wala kumwandikia barua ya kumtaka afanye hivyo.

“Hajawahi kuniletea barua rasmi ya kutaka niombe msamaha. Nimekuwa nikimsikia na kumuona akizungumza kupitia mitandao ya kijamii, na siwezi kufuatilia jambo hilo kwa msingi huo,” amesema Nondo.

Amesema kauli anazotuhumiwa kuzitoa kuhusu uchaguzi wa mwaka 2025 si maoni yake binafsi pekee, bali ni hoja ambazo zimekuwa zikizungumzwa na baadhi ya wananchi wa Kigoma pamoja na wadau wengine kuhusu mwenendo wa uchaguzi huo.

“Nimezungumza, lakini hayo ni maneno yanayozungumzwa na wananchi wa Kigoma. Siyo wananchi pekee, hata baadhi ya waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi walitoa maoni yao kuhusu uchaguzi huo,” amesema.

Hata hivyo, Nondo amedai kuwa yeye alimwandikia Baba Levo barua ya kumtaka aombe msamaha, na kwamba asipofanya hivyo atafungua kesi ya madai mahakamani akimtaka kulipa fidia ya Sh500 milioni kwa madai ya kumchafua na kumdhalilisha.

Amesema barua hiyo ilitolewa tangu Mei 23, 2026, baada ya kuzungumza na vyombo vya habari, lakini muda alioutoa kwa Baba Levo kutekeleza matakwa hayo umeshapita.

Kwa mujibu wa Nondo, mbunge huyo amekuwa akitamka na kusambaza taarifa za uongo dhidi yake katika nyakati tofauti, hususan madai ya kujiteka mwenyewe, jambo ambalo anasema lilishatolewa uamuzi na mahakama na kuthibitisha kuwa hana hatia.

Wakili wa Nondo, Hekima Mwasipu, amesema muda waliompa Baba Levo wa kuomba msamaha umekwisha, hivyo wanatarajia kufungua kesi hiyo kesho Jumatatu Juni 1, 2026, jijini Dar es Salaam.

“Kesho Jumatatu tunafungua kesi hiyo Dar es Salaam kwa sababu tulimpa muda wa kuomba msamaha, lakini muda huo umeisha bila kutekeleza matakwa yetu,” amesema Mwasipu.

Kwa upande wake, Baba Levo amesema Nondo naye ameshindwa kuomba msamaha ndani ya muda aliopangiwa, hivyo hatua iliyobaki ni kuziacha mamlaka husika zifanye kazi yake.

“Tuache sheria ifuate mkondo wake. Hataki kuniomba msamaha na muda niliompa umeisha, kwa hiyo tuwaachie wanasheria wafanye kazi. Nitamfikisha mahakamani ili athibitishe maneno anayoyasema,” amesema.

Mbunge huyo amesema maandalizi ya kufungua shauri hilo yanaendelea kupitia wakili wake, akisisitiza lengo lake ni kuona Nondo anathibitisha madai anayoyatoa hadharani.

“Anapaswa kuthibitisha kauli zake. Nikimuacha bila kuchukua hatua, watu wanaweza kuona jambo hilo ni la kawaida,” amesema.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports