Ndoa siyo nyumba ya wageni bali nyumba ya wawili

Canada. Kuna mazoea na mila za kimaskini na kinyonyaji hasa katika baadhi ya jamii linapokuja suala la ndoa.  Unakuta binti kaolewa jana, kesho yake, ndugu zake wanahamia kwake. Watu hata hawajajuana kitabia, ndugu wameishaanza kujisomba na kujijaza.  Ndoa siyo nyumba ya wageni au ustawi wa jamii. Japo si vibaya kuwakirimu na kuwatunza ndugu, wengine wanazidisha.…

admin Avatar

by

3 minutes

Read Time

Canada. Kuna mazoea na mila za kimaskini na kinyonyaji hasa katika baadhi ya jamii linapokuja suala la ndoa. 

Unakuta binti kaolewa jana, kesho yake, ndugu zake wanahamia kwake. Watu hata hawajajuana kitabia, ndugu wameishaanza kujisomba na kujijaza.

 Ndoa siyo nyumba ya wageni au ustawi wa jamii. Japo si vibaya kuwakirimu na kuwatunza ndugu, wengine wanazidisha.

Zipo jamii zetu ambazo kwao, kuolewa kwa ndugu yao ni kupata mahali pa kuponea kimaisha. Utasikia mara “kaka kafukuzwa shule hana karo. Mara bibi anaumwa na hana fedha ya matibabu. Hivyo, baba na mama wanaomba tumuwezesha.”

Si vibaya kama mna uwezo wa kufanya hivyo. Hata hivyo, na wahusika waone aibu. Hamjamuozesha mwanenu ili awe kitega uchumi jamani.

 Mbali na utegemezi, kuna mazoea mengine ya ovyo ambayo yanaweza kulea uvivu na ukosefu wa ubunifu na kujitegemea kwa wanaoendekeza kutumia ndoa kama sehemu ya kuponea mbali na kudhoofisha hata kuvunja ndoa.

Mfano, binti kaolewa mjini. Kila atokaye kwao kijijini kwenda mjini anageuza kwa binti kuwa kwake. Badala ya ndoa kuwa sehemu ya wawili kuanza maisha, inageuka nyenzo na sehemu ya baadhi ya watu wavivu na wakosefu wa ubunifu na staha kuingilia mjini. Tulishaambiwa kuwa mtegemea cha nduguye hufa maskini.

Wengine huenda kwa ndugu zao hata bila kutoa taarifa mbali na kutokuwa na mipango ya kujitegemea wafikapo hasa mjini.

Utakuta watu wameona juzi. Ndiyo wanaanza maisha. Saa nyingine wamepanga chumba kimoja au viwili. Halafu watu wanakuja kujazana na kufanya ndoa iwe karaha.

Huku si kunyonyana tu bali hata kuumizana na kubebeshana mizigo isiyo ya lazima. Yanini yote haya? Mtatunza wangapi? Ukienda mjini, nenda na malengo na mipango yako na siyo kutegemea shemeji au dada awe daraja la kukuvusha.

 Japo wapo waathirika wengi wa mchezo huu wasiolalamika, yanawakumba wengi na wanaumia kimya kimya. Waathirika wengi huona aibu au kuogopa watachukiwa na kuitwa wabinafsi na wachoyo.

Kulinda ndoa yenu si ubinafsi wala uchoyo bali ni stahiki na wajibu kwenu. Kila mtu lazima ajue atakavyoyaishi maisha yake.

Japo tunatumia maneno yenye ukakasi kidogo, kwetu, huu ni unyanyonyaji. Hatuna jina la kuupa zaidi ya kuuita unyonyaji. Wengi wa wanaoendekeza mambo haya ni wavivu wa kutafuta.

Wanapungukiwa staha na ubunifu wa kujitafutia maisha. Mbali na ubinafsi, utegemezi, na uvivu wa kutafuta, vyanzo vikuu vya janga hili ni ujinga na ukosefu wa staha. Utakuta baba zima limemaliza, tuseme, chuo au sekondari, bila aibu, linakimbilia kwa shemeji na kuweka makao kiasi cha kusahau hata kuchakarika.

Wanaoendekeza ujinga na unyonyaji huu hawawasaidii wahusika bali kutengeneza umaskini wa kujitakia.

Ukitaka kujua madhara ya mchezo au tabia hii, acha ndoa ivunjike. Wale wale waliokirimiwa ndiyo wa kwanza kumlaumu mhusika wasijue nao wanaweza kuwa sababu ya kuvunjika au kutofana kwa  ndoa.

 Tulishaonya. Wema usizidi uwezo. Japo si vibaya kuomba msaada kwa ndugu, ila ndugu wengine wanazidi kiasi cha kuweza hata kuharibu ndoa za ndugu zao.

Kuna kisa kimoja tunakijua fika. Binti mmoja aliolewa na jamaa mwenye uwezo si haba. Acha ndugu wajazane. Kila siku, mara baba au mama au shangazi anataka msaada. Mara shemeji yako kamaliza kidato cha sita na hana kazi, hivyo, atakuja mjini mtafutie kazi.

Ndoa siyo taasisi ya kuondoa ndugu kwenye umaskini. Kuna haja ya kuwaacha wanandoa wahangaikie ndoa na maisha yao. Kama wataona wana uwezo wa kusaidia ndugu, wafanye hivyo kwa kutaka na siyo kulazimika.

Wengine, hasa mashemeji wa kike, huanza kujipitishapitisha kwa shemeji yao wamtie vishawishi. Wapo pia wanaotaka wavuruge hata ndoa ya ndugu yao kisa kapata mwenye uwezo. Kama unataka mwenye uwezo, si utafute wako kama ni rahisi kihivyo.

Hali huwa mbaya pale shemeji mwenyewe akiwa ni kiwembe au anatoka kwenye jamii ambazo zina msemo kuwa ‘shemegi’ tunakulaga. Kwani hayapo?

Tumalizie kwa kusema kuwa tumeyaandika haya si kwa roho mbaya wala kufundisha wanandoa wasiwasaidie ndugu zao.

La hash!. Lengo ni kuyagusa yasiyogusika au yanayofumbiwa macho lakini yakawa na madhara fiche tena makubwa. Ndoa siyo nyumba ya wageni bali nyumba ya wawili.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports