‘Taasisi imara msingi ukuaji wa uchumi Afrika’

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa ukuaji wa uchumi wa Afrika utategemea uwezo wa nchi zake kujenga taasisi imara zinazoweza kuimarisha imani ya wawekezaji, kuvutia mitaji ya muda mrefu na kuelekeza fedha katika sekta za uzalishaji. Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Plc, Ruth Zaipuna, alipohutubia Kongamano la Cambridge…

admin Avatar

by

3 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa ukuaji wa uchumi wa Afrika utategemea uwezo wa nchi zake kujenga taasisi imara zinazoweza kuimarisha imani ya wawekezaji, kuvutia mitaji ya muda mrefu na kuelekeza fedha katika sekta za uzalishaji.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Plc, Ruth Zaipuna, alipohutubia Kongamano la Cambridge Africa Business Conference 2026 lililobeba kaulimbiu ya “Kujenga Mustakabali wa Afrika: Mitaji, Ubunifu na Ukuaji wa Pamoja wa Bara la Afrika.”

Kupitia hotuba hiyo, Zaipuna aliiweka Tanzania na NMB katika mjadala mpana uliowakutanisha wasomi, wawekezaji, watunga sera, taasisi za fedha za maendeleo na viongozi wa biashara waliokuwa wakijadili mustakabali wa uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.

“Mustakabali wa Afrika hautaletwa na wengine, utajengwa na Waafrika wenyewe kupitia mifumo jumuishi, taasisi zinazoaminika na nidhamu ya kuhakikisha matokeo chanya na endelevu kwa vizazi vijavyo,” amesema.

Akizungumzia  safari ya mafanikio ya NMB, akitumia kama mfano safari ya ukuaji wake katika mjadala huo Zaipuna amesema benki hiyo ilianza mwaka 1997 ikiwa na matawi 97, wateja takribani 600,000 na amana za Sh150 bilioni.

Hata hivyo, kupitia uwekezaji wa kimkakati na mageuzi ya muda mrefu, imekua na kuwa miongoni mwa taasisi kubwa za kifedha nchini.

Amesema mafanikio hayo yamejengwa katika misingi ya utawala bora, nidhamu ya utekelezaji, uwekezaji kwa rasilimali watu na teknolojia pamoja na dhamira ya kuendeleza ujumuishi wa kifedha.

“Kati ya mwaka 2021 na 2025, tumewekeza zaidi ya Sh230 bilioni katika miundombinu ya kidijitali, usalama wa mifumo, teknolojia za kiotomatiki na matumizi ya takwimu. Matokeo yake, zaidi ya asilimia 98 ya miamala yote kwa sasa inafanyika nje ya matawi kupitia njia za kidijitali na mbadala,” amesema.

Amesema idadi ya wateja wa NMB imeongezeka na kufikia zaidi ya milioni 10, huku benki hiyo ikirekodi faida kabla ya kodi ya Sh1.1 trilioni mwaka 2025 na kuwa kampuni ya kwanza nchini Tanzania kuvuka kiwango hicho cha faida.

Kwa mujibu wa Zaipuna, mali za benki zilifikia Sh17.2 trilioni, mikopo na rasilimali kwa wateja zikizidi Sh10.6 trilioni, huku amana zikifikia Sh12.6 trilioni.

Amesema ukuaji huo haupaswi kupimwa kwa kiwango cha faida pekee, bali pia kwa mchango wake katika kukuza uchumi halisi wa Tanzania.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, NMB imetoa takribani Sh28 trilioni katika uchumi wa nchi kupitia ufadhili wa sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, viwanda, biashara, nishati, miundombinu na kaya.

Mbali na hilo, benki hiyo imechangia takribani Sh2.7 trilioni katika kodi za Serikali na kuwekeza katika miradi ya afya, elimu, uwezeshaji wa vijana na uhifadhi wa mazingira.

Zaipuna pia alizitaja hati fungani za Jasiri na Jamii zilizokusanya jumla ya Sh474 bilioni kuwa ushahidi wa uwezo wa masoko ya mitaji ya Afrika katika kukusanya fedha kwa kiwango kikubwa huku yakichochea ujumuishi wa kifedha na maendeleo endelevu.

Akichangia mjadala huo, mtaalamu wa fedha kutoka AfDB, Eghosa Giwa Osaige, amesema kuimarisha uaminifu na kupunguza gharama za vihatarishi vya uwekezaji ni hatua muhimu zitakazosaidia kuongeza mtiririko wa mitaji kuelekea Afrika na kufungua fursa za uwekezaji wa muda mrefu.

Naye Mkurugenzi wa Uwekezaji wa BII, Jumai Mohammed, amesema hati fungani za kijamii na uendelevu za NMB zimeonyesha namna ubunifu, ushirikiano na masoko ya mitaji vinavyoweza kufungua uwekezaji mkubwa na kuwa mfano kwa taasisi nyingine za kifedha barani Afrika.

“BII itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Afrika katika kuhamasisha mitaji yenye matokeo chanya kwa maendeleo ya bara hili,” amesema.

Kauli ya Zaipuna imekuja wakati nchi nyingi za Afrika zikiendelea kutafuta vyanzo vya fedha za muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji katika miundombinu, nishati, usafirishaji, kilimo, teknolojia na sekta nyingine za uzalishaji zinazochochea ukuaji endelevu wa uchumi wa bara hilo.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports