KAMATI YA BUNGE YA AFYA YAIPONGEZA BMH KWA MAFANIKIO YA HUDUMA ZA UBINGWA BOBEZI – Habari Mpya

Na Meleka Kulwa, Fullshangwe Blog – Dodoma Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeipongeza Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, ikisema hospitali hiyo imekuwa kituo muhimu cha rufaa kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu maalumu nchini. Pongezi…

admin Avatar

by

2 minutes

Read Time

Na Meleka Kulwa, Fullshangwe Blog – Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeipongeza Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, ikisema hospitali hiyo imekuwa kituo muhimu cha rufaa kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu maalumu nchini.

Pongezi hizo zimetolewa Juni 9, 2026 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Johannes Lukumay, wakati wa ziara ya kamati kukagua maendeleo ya hospitali hiyo, ikiwemo ujenzi wa jengo la matibabu ya saratani, pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa.

Dkt. Lukumay amesema uboreshaji wa huduma chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi, umeifanya hospitali hiyo kuwa miongoni mwa vituo vinavyoongoza kwa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi nchini. Ameipongeza pia kwa mafanikio ya huduma ya upandikizaji uloto, ambayo tayari imenufaisha watoto 30 wenye umri wa miaka 4 hadi 12.Amesema Serikali inapaswa kuendelea kuimarisha mifumo ya kugharamia matibabu ya magonjwa sugu kama saratani, figo, moyo, kisukari na magonjwa ya mifupa ili kuhakikisha huduma zinapatikana kwa wakati.

Aidha, Dkt. Johannes Lukumay amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Prof. Abel Makubi, kwa kazi kubwa ya kuboresha huduma za afya hospitalini hapo, akibainisha kuwa uongozi wake umeiwezesha hospitali hiyo kupiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma. Amesema ameona mabadiliko makubwa yanayoendelea hospitalini hapo na kuongeza kuwa uongozi wa Prof. Makubi umeonyesha maono na uthubutu katika kuimarisha huduma kwa wananchi, huku akiwapongeza watumishi wa hospitali hiyo kwa weledi na juhudi zao katika kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora kwa wakati.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema uwekezaji wa Serikali umeiwezesha BMH kutoa huduma za kibingwa 20 na ubingwa bobezi 17. Amesema mafanikio hayo yamechangiwa pia na programu za mafunzo kwa wataalamu kupitia Samia Scholarship.

Ameongeza kuwa Serikali imetenga shilingi bilioni 33 kwa ujenzi wa jengo la saratani na shilingi bilioni 4 kwa ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa. Amesisitiza umuhimu wa wananchi kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kupitia kampeni ya “Jue Namba Zako”.Awali akizungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi, amesema hospitali hiyo imeboresha huduma na kupunguza muda wa kusubiri wagonjwa kutoka siku 2–3 hadi kati ya saa 3–6. Amesema pia hospitali ina huduma za kibingwa 20 na ubingwa bobezi 17 zikiwemo upasuaji wa moyo kwa watoto, upandikizaji figo, na matibabu ya mfumo wa mkojo kwa teknolojia ya kisasa.

Aidha, amesema hospitali imeimarisha mifumo ya huduma kwa wateja kupitia kituo cha simu cha saa 24 na njia za mawasiliano za kidijitali, huku maabara yake ikiwa na ithibati ya kimataifa kwa mara ya tatu mfululizo.

Prof. Makubi ameongeza kuwa BMH inalenga kuwa Hospitali ya Taifa kutokana na kupanuka kwa huduma zake, huku ikiendelea na miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Figo kwa ufadhili wa Serikali ya Japan (shilingi bilioni 28) pamoja na mpango wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports