Leo hii, Trash to Treasure hukusanya taka za plastiki kutoka katika jamii na kuzibadilisha kuwa vifaa vya kujifunzia vinavyosaidia watoto kujifunza kwa njia rahisi, ya kuvutia na ya vitendo. Lakini safari hiyo haikuanza kama biashara kubwa. Ilianza na swali moja rahisi lakini lenye maana kubwa.
Mwaka 2021, mwanzilishi wa Trash to Treasure alijiuliza:
“Vipi kama hiki kitu tunachokiita taka kinaweza kuwa fursa?”
Kwa wengi, taka ilikuwa uchafu usio na thamani. Lakini kwake, ndani ya taka kulikuwa na uwezekano wa kubadili maisha ya watu wengine, hasa watoto waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia.
Mwanzilishi huyo anatoka katika familia ya kipato cha chini. Akiwa mtoto, mazingira ya kujifunzia hayakuwa rahisi. Vifaa vya kujifunzia vilikuwa vichache, hivyo yeye pamoja na watoto wengine walijifunza kwa kutumia vijiti, vizibo vya soda na vitu vya kawaida vilivyopatikana mazingira ya karibu kama njia ya kujifunzia herufi na namba.
Hata hivyo, kulikuwa na jambo jingine lililomgusa zaidi.
Kila mvua iliponyesha, maji yalifurika yakiwa yamebeba taka nyingi za plastiki. Taka hizo zilienea kila mahali na kuacha mazingira machafu, hususan karibu na maeneo ya watoto kuchezea.
Kila jioni baada ya shule, yeye na marafiki zake walikuwa wakielekea uwanjani kucheza mpira huku kila mmoja akiwa na ndoto ya kuwa kama Ronaldo. Karibu na uwanja huo kulikuwa na mtaro mdogo uliokuwa ukijaa taka za plastiki kila mvua iliponyesha.
Kwa mtoto mdogo, hilo lilionekana kama kero ya kawaida. Lakini miaka kadhaa baadaye, jambo hilo hilo liligeuka kuwa chanzo cha suluhisho kubwa.
Hapo ndipo safari ya Trash to Treasure ilipoanza.
Wazo halikuwa tu kuondoa taka kwenye mazingira. Wazo kubwa lilikuwa kuzibadilisha taka hizo kuwa vitu vinavyoweza kubadili maisha ya watoto wengine.
“Taka ni mali.”
Hiyo si kaulimbiu tu ya Trash to Treasure iliyopo Sumbawanga mkoani Rukwa, bali ni falsafa ya maisha na safari iliyoanzia kwenye kumbukumbu za utoto.
Leo hii, taka za plastiki zinazokusanywa huzichambuliwa, kusafishwa na kuchakatwa kabla ya kubadilishwa kuwa vifaa mbalimbali vya elimu vinavyorahisisha ujifunzaji kwa vitendo.
Miongoni mwa vifaa vinavyotengenezwa ni herufi za kujifunzia, namba, meno ya mfano, fuvu la kichwa cha binadamu, mifupa ya mfano pamoja na vifaa vingine vinavyowasaidia watoto wa kawaida na wale wenye mahitaji maalum kujifunza na kucheza kwa urahisi zaidi.
Mpaka sasa, Trash to Treasure imefanikiwa kutengeneza zaidi ya katoni 320 za vifaa vya kujifunzia herufi na namba, pamoja na zaidi ya vifaa 400 vya mifano ya kujifunzia kama mifupa ya binadamu, meno, fuvu la kichwa na vifaa vingine vya kielimu.
Lengo kuu ni kuifanya elimu iwe rahisi, ya kuvutia na yenye kugusa maisha halisi ya watoto.
Hata hivyo, safari hiyo haikuwa rahisi.
Kabla ya kushiriki katika programu ya Regenerative Economy Accelerator Tanzania (REAT), Trash to Treasure tayari ilikuwa ikifanya kazi nzuri kupitia ushirikiano wa jamii na kampeni mbalimbali za mazingira. Lakini ukuaji wake ulikuwa na changamoto nyingi.
Mfumo wa kazi ulikuwa wa kawaida, matokeo yalikuwa magumu kupimika, na mipango ya muda mrefu haikuwa imejengwa kwa msingi imara.
Kupitia programu ya REAT, mabadiliko makubwa hayakuwa tu kujifunza namna bora ya kuchakata taka.
Mabadiliko makubwa zaidi yalikuwa kubadilika kwa mtazamo.
Kutoka kujiuliza:
“Tunawezaje kuchakata taka?”
Mpaka kufikia swali kubwa zaidi:
“Tunawezaje kujenga mfumo unaobadilisha mazingira, elimu, uchumi na maisha ya watu kwa wakati mmoja?”
Hicho ndicho kinachoitwa kubadili tatizo kuwa suluhisho.
Baada ya kuimarisha mfumo wake wa biashara kupitia mtazamo wa uchumi rejeshi, Trash to Treasure imefanikiwa kuongeza mara mbili uwezo wake wa kukusanya taka za plastiki.
Kwa sasa, kampuni hukusanya takriban tani 14 za plastiki kwa mwaka.
Kati ya Oktoba na Desemba mwaka 2025, kiwango cha plastiki kilichochakatwa kiliongezeka kwa kiasi kikubwa huku biashara hiyo ikizalisha zaidi ya shilingi milioni 28 kwa mwaka.
Matokeo yalianza kuonekana wazi.
Plastiki ambayo zamani ingeendelea kuchafua mazingira kwa miaka mingi sasa inarudi kwenye mzunguko wa thamani kwa kuzalisha vifaa vya kujifunzia vinavyorahisisha elimu kwa vitendo.
Kupitia kampeni za mara kwa mara za kuokota taka katika mitaa mbalimbali, jamii nayo ilianza kubadilika.
Watu ambao zamani walikuwa wakipita pembeni ya taka bila kuziona, sasa wameanza kuzitambua kama rasilimali yenye thamani. Wengine wameanza kuzikusanya na kuziuza kwa Trash to Treasure kama chanzo kipya cha kipato.
Leo hii, mfumo huo wa uchumi rejeshi umegeuka kuwa chanzo cha ajira na kipato kwa jamii.
Trash to Treasure inafanya kazi na wakusanyaji wa plastiki 20 kutoka Sumbawanga na Kigoma. Aidha, imeajiri wafanyakazi 12 wa kudumu pamoja na kutoa fursa kwa wanawake 10 wanaojihusisha na uchambuaji wa plastiki kabla ya kuingia kwenye hatua ya uchakataji.
Kwa baadhi yao, kitu kilichokuwa kikionekana kama taka sasa kimekuwa sehemu ya kujenga maisha.
Kwa vijana na wanawake wengi, mfumo huo umefungua fursa mpya za kipato na uhakika wa maisha.
Kwa shule, umekuwa njia ya kupata vifaa vya kujifunzia vya gharama nafuu, vinavyodumu muda mrefu na vinavyorahisisha ujifunzaji.
Mpaka sasa, Trash to Treasure imefikia shule 32 katika maeneo ya Iringa, Sumbawanga na Kigoma.
Ndoto ya kuona watoto wa Kitanzania wakijifunza kwa kutumia vifaa vinavyowafanya waipende shule zaidi inaendelea kukua kila siku.
Lakini hii bado ni hatua ya mwanzo.
Tanzania ina zaidi ya shule 28,000, huku shule nyingi zikiendelea kuhitaji vifaa bora vya kujifunzia, hasa kwa watoto wenye mahitaji maalum.
Mahitaji bado ni makubwa kuliko uwezo wa sasa wa uzalishaji.
Lakini ndani ya changamoto hiyo kuna ndoto kubwa zaidi.
Ndoto ya kuona jamii zikibadilisha mtazamo na kuanza kuona taka si kama uchafu, bali kama rasilimali yenye uwezo wa kujenga maisha.
Kwa sababu mwisho wa siku, taka si mwisho wa hadithi.
Wakati mwingine, ndiyo mwanzo wa hadithi mpya kabisa.













