Ktoka mitaa ya Magomeni jijini Dar es Salaam hadi Ikulu ya Windhoek nchini Namibia, safari ya maisha ya Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah ni moja ya simulizi za kipekee katika historia ya harakati za ukombozi barani Afrika.
Miaka kadhaa kabla ya Namibia kupata uhuru wake mwaka 1990, Netumbo alikuwa miongoni mwa wanaharakati wa SWAPO waliolazimika kuishi uhamishoni kutokana na mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Katika kipindi hicho, Tanzania ilitoa hifadhi kwa wapigania uhuru kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika, na Netumbo aliwahi kuishi Magomeni jijini Dar es Salaam, eneo ambalo lilikuwa sehemu ya maisha yake wakati wa harakati hizo.
Kumbukumbu za maisha hayo zimeendelea kubaki hai hata baada ya kupanda ngazi za juu za uongozi nchini Namibia. Alipotembelea Tanzania kwa mara ya kwanza akiwa Rais wa Namibia mwezi Mei 2025, Netumbo alipata fursa ya kukutana tena na baadhi ya majirani zake wa zamani aliokuwa akiishi nao Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam katika miaka ya 1980. Miongoni mwao walikuwa Bi. Salama Salehe Ghulum (Mama Salehe) na Bi. Rafran Ismail Khan.
Rais Nandi alikutana na majirani zake katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa Ikulu jijini Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 20 Mei 2025. Tukio hilo lilionesha namna Tanzania ilivyobaki kuwa sehemu muhimu ya safari yake ya maisha, kutoka enzi za harakati za ukombozi hadi kufikia nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa taifa la Namibia.
Leo, baada ya miongo kadhaa ya mapambano, diplomasia na uongozi wa umma, Kiongozi huyo mwanamke ambaye aliwahi kuwa sehemu ya harakati za ukombozi wa nchi yake wakati akiishi nchini Tanzania ndiye Rais wa Namibia.
Hivyo, ziara yake nchini Tanzania kuanzia Juni 19 hadi 21, 2026, si ziara ya kawaida ya kidiplomasia bali ni safari inayomrudisha katika moja ya maeneo yaliyoshuhudia sehemu ya maisha yake wakati wa mapambano ya uhuru.
Ziara hiyo inabeba kumbukumbu za historia ya pamoja kati ya Tanzania na Namibia, mataifa mawili yaliyounganishwa na harakati za ukombozi wa Afrika. Aidha, inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji katika kipindi ambacho nchi zote mbili zinaelekeza nguvu katika maendeleo ya wananchi wake.
Ziara ya Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania ni tukio la kihistoria, kisiasa na kiuchumi. Ziara hiyo inakuja wakati nchi hizi mbili zikiendelea kuimarisha mahusiano yao yaliyojengwa katika misingi ya mshikamano wa harakati za ukombozi wa Afrika.
Netumbo Nandi-Ndaitwah ni miongoni mwa viongozi wachache wa Afrika ambao historia yao imejengwa katika mapambano ya uhuru. Kupitia chama cha SWAPO, alishiriki harakati za ukombozi wa Namibia dhidi ya utawala wa kikoloni wa Afrika Kusini na baadaye akashika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika serikali ya Namibia hadi kufikia kuwa Rais wa taifa hilo mwaka 2025. Safari hiyo ya kisiasa imeifanya kuwa miongoni mwa viongozi wenye uelewa mpana wa historia ya ukombozi na maendeleo ya Afrika.
Kwa Namibia, Tanzania haikuwa tu mshirika wa kidiplomasia bali ilikuwa ngome ya harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika. Chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania ilitoa hifadhi, mafunzo na msaada wa kisiasa kwa wapigania uhuru wa Namibia kupitia SWAPO.
Historia hiyo ndiyo inayofanya ziara ya Netumbo kuwa na maana ya kipekee. Ni safari inayomrudisha katika taifa ambalo lilichangia kwa kiasi kikubwa mapambano yaliyoiwezesha Namibia kupata uhuru mwaka 1990. Aidha, ni kurejea katika nchi aliyowahi kuishi wakati wa kipindi kigumu cha mapambano ya ukombozi, jambo linaloipa ziara hiyo uzito wa kihistoria unaozidi ule wa diplomasia ya kawaida.
Ziara hiyo pia inafanyika wakati Tanzania inaongozwa na Rais , kiongozi ambaye ameendeleza kwa nguvu diplomasia ya uchumi, biashara na uwekezaji. Hivyo, ziara hiyo inawakutanisha kihistoria nchi mbili zenye urafiki wa muda mrefu na maono yanayofanana kuhusu maendeleo ya Afrika.
Muhimu zaidi, ziara hii inabeba ishara ya kuimarisha nafasi ya wanawake katika uongozi wa Afrika. Rais Mhe. Dkt. Samia na Rais Mhe. Netumbo ni miongoni mwa wanawake wachache waliofikia nafasi za juu kabisa za uongozi katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, jambo linaloonesha mabadiliko makubwa ya kisiasa yanayoendelea katika bara hili.
Tangu alipoingia madarakani mwaka 2025, Netumbo ameanza mageuzi yanayolenga kuongeza ufanisi wa serikali kwa kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri, kuimarisha uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Mageuzi hayo yanaendana na juhudi za Tanzania za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Kwa upande wa uchumi, viongozi hawa wawili wanaonekana kushirikiana katika falsafa ya kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zao zinawanufaisha wananchi. Namibia imeelekeza nguvu katika mafuta, gesi, madini na nishati safi, huku Tanzania ikiendelea kuimarisha sekta za madini, gesi asilia, kilimo na utalii.
Katika miaka ya hivi karibuni, mahusiano ya Tanzania na Namibia yameanza kuhamia zaidi katika diplomasia ya uchumi. Wakati historia yao ilijengwa katika mshikamano wa kisiasa, sasa msingi wake unapanuliwa kuelekea biashara, uwekezaji, teknolojia na maendeleo ya sekta binafsi.
Sekta ya madini ni moja ya maeneo yenye fursa kubwa zaidi za ushirikiano. Namibia imejijengea sifa katika usimamizi wa sekta ya almasi, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika. Ushirikiano wa kitaalamu unaweza kusaidia kuongeza thamani ya rasilimali hizo ndani ya nchi kabla ya kuuzwa nje.
Katika sekta ya nishati, ugunduzi wa mafuta na gesi nchini Namibia unafungua fursa mpya za ushirikiano. Tanzania, ambayo ina uzoefu mkubwa katika usimamizi wa gesi asilia, inaweza kuwa mshirika muhimu katika kubadilishana uzoefu wa sera, sheria na usimamizi wa rasilimali hizo.
Aidha, Namibia imekuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza Afrika katika uwekezaji wa nishati safi hususan Green Hydrogen. Hili ni eneo ambalo linaweza kufungua milango ya ushirikiano mpya kati ya nchi hizi mbili katika uchumi wa kijani unaokua kwa kasi duniani.
Nchi zote mbili pia zinanufaika na uanachama wao katika (SADC) na , mifumo inayolenga kuongeza biashara ya ndani ya Afrika kwa kuondoa vikwazo vya kibiashara.
Kupitia AfCFTA, Tanzania inaweza kupanua zaidi masoko ya bidhaa zake katika Kusini mwa Afrika, huku Namibia ikipata fursa ya kutumia Tanzania kama lango muhimu kuelekea soko la Afrika Mashariki. Hii ni hatua muhimu katika kujenga uchumi wa Afrika unaojitegemea zaidi.
Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Walvis Bay ya Namibia zinaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuunganisha biashara kati ya Mashariki na Kusini mwa Afrika. Ushirikiano wa kimkakati katika miundombinu ya usafirishaji unaweza kuongeza ushindani wa bidhaa za nchi hizo mbili katika soko la bara.
Kwa ujumla, ziara ya Netumbo Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania ni zaidi ya ratiba ya kidiplomasia. Ni mwendelezo wa urafiki uliojengwa katika harakati za ukombozi na unaoelekezwa sasa katika ajenda ya maendeleo ya kiuchumi, biashara na uwekezaji. Kwa Netumbo binafsi, ziara hii pia ni kurejea katika nchi ambayo ilikuwa sehemu ya safari yake ya maisha wakati wa mapambano ya uhuru wa Namibia.
Iwapo mazungumzo yatakayofanyika yatazaa mikakati mipya ya ushirikiano, ziara hii inaweza kuwa hatua muhimu katika kufungua ukurasa mpya wa mahusiano ya Tanzania na Namibia, ambapo urithi wa ukombozi utaunganishwa na fursa za uchumi wa kisasa kwa manufaa ya wananchi wa mataifa yote mawili.













