MAHUBIRI: Thamani ya fursa unayopewa na Mungu

Bwana Yesu asifiwe! Karibu kwenye tafakari ya neno la Mungu leo Jumapili. Tumepewa kichwa cha somo kinachosema Thamani ya fursa unayopewa na Mungu. Msingi wa somo letu unatoka kwenye Kitabu cha Mwanzo Mwanzo 27:34-40.  Katika safari ya maisha ya kila binadamu, Mungu hutupatia fursa mbalimbali. Fursa hizi zinaweza kugawanywa katika makundi mawili makuu: fursa zinazojirudia…

admin Avatar

by

6 minutes

Read Time

Bwana Yesu asifiwe! Karibu kwenye tafakari ya neno la Mungu leo Jumapili. Tumepewa kichwa cha somo kinachosema Thamani ya fursa unayopewa na Mungu. Msingi wa somo letu unatoka kwenye Kitabu cha Mwanzo Mwanzo 27:34-40.

 Katika safari ya maisha ya kila binadamu, Mungu hutupatia fursa mbalimbali. Fursa hizi zinaweza kugawanywa katika makundi mawili makuu: fursa zinazojirudia na fursa zisizojirudia. Fursa zisizojirudia ni zile zinazojitokeza mara moja tu katika maisha yetu, na mara tu zinapopotea, hazirudi tena. Gharama ya kupoteza fursa kama hizi ni kubwa sana, kwani huwezi kurejea katika hali uliyotamani kuwa nayo kama ungetumia fursa hiyo kwa busara.

Makala hii inalenga kutuongoza katika kuelewa thamani ya fursa tunazopewa na Mungu, hasa zile zinazojitokeza mara moja, kwa kutumia mfano halisi kutoka katika Maandiko Matakatifu-simulizi ya maisha ya Esau na Yakobo.

Kuna fursa nyingi ambazo Mungu hutupatia katika maisha yetu, lakini baadhi yake ni za thamani kubwa kwa sababu hazijirudii. Hizi ni pamoja na:

Fursa ya kuzaliwa na kukua katika familia fulani – Huwezi kuchagua tena wazazi wako au mazingira ya utoto wako. Hii ni fursa ambayo hutukeaa mara moja tu.

Fursa ya elimu ya awali – Wakati wa utoto, tunajifunza lugha, tabia, na stadi za msingi. Wakati huu haurudishwi.

Fursa ya kukutana na mtu fulani kwa mara ya kwanza -Hisia na matukio ya “mara ya kwanza” hayawezi kurudiwa kwa usawa uleule.

Fursa ya kufanya uamuzi muhimu kwa wakati maalum – Kama kukubali ofa ya kazi, kuomba msamaha kwa mtu kabla hajafa, au kuchukua hatua ya uwekezaji katika wakati muafaka.

Fursa ya kuishi sasa – Kila siku ni fursa inayokuja mara moja; wakati unaopita haurudi.

Fursa ya umri wa uvulana na usichana – Maisha kabla ya kuingia katika mahusiano ya ndoa yana thamani kubwa, hasa kwa usafi wa moyo usio na hatia.

ESAU NA FURSA YA MZALIWA WA KWANZA

Simulizi ya Esau na Yakobo ni kielelezo bora cha jinsi fursa inavyoweza kutumika au kupotezwa. Esau alikuwa na nafasi kubwa kama mzaliwa wa kwanza, fursa ambayo ingempa:

Haki ya kubeba jina la ukoo

Kupokea sehemu mara mbili ya urithi (double portion)

Kulinda hatma ya familia kwa kukomboa mjane, mtumwa, au ardhi ya familia

Tabia za Fursa Ambazo Esau hakuwa Makini nazo.

Fursa ina tabia zake ambazo ni muhimu kuzielewa:

Unapopoteza fursa, haipotei bure – Inaenda kwa anayeitumia vyema

Inashindaniwa na watu zaidi ya mmoja

Matumizi ya Esau ya fursa yake

Maisha ya Esau yanaweza kugawanywa katika sehemu nne kuu:

Alipata fursa ya mzaliwa wa kwanza – Alizaliwa  wa kwanza na akaiipigania tangu akiwa tumboni. Mungu alimwambia mama yao Rebeka: “Mataifa mawili yanashindana tumboni mwako” (Mwanzo 25:23).

Aliitazama kwa mazoea na kuidharau -Aliuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa bakuli la supu akiwa na miaka 20, aliiidharau thamani yake (Mwanzo 25:32-33).

Alipoteza mbaraka wa mzaliwa wa kwanza – Miaka 20 baadaye, Yakobo na mama yake Rebeka walimdanganya Isaka na kupokea mbaraka uliokuwa wa Esau (Mwanzo 27).

Aliipambania kurejesha nafasi yake – Ingawa mwanzoni alitaka kumuua Yakobo, baada ya miaka 20 alikutana naye na hawakugombana. Hata hivyo, vizazi vyao viliendeleza uadui, kwani nafasi ya wazao wa Yakobo ilikuwa mbele zaidi ya wazao wa Esau (Edomu).

Kutokana na simulizi hii, tunaona kwamba Esau:

Alidharau fursa kwa kuendekeza njaa na tumbo lake

Alifanya uzembe kwa kuchukulia kawaida mapatano na mdogo wake

Alijiamini kuwa hangeweza kupoteza fursa hiyo

Maombi ya Esau na uchungu wa kupotea fursa

Esau alipogundua kuwa amepoteza mbaraka wake, alilia kwa uchungu (Mwanzo 27:34). Maombi yake yanaonyesha mambo matatu muhimu:

Uchungu wa kupoteza fursa – Tambua uchungu huo, kwani unaweza kuwa fursa ya kurejesha kilichopotea.

Shauku ya kupata fursa mpya – Huu ndio ufunguo wa kuanza upya.

Umakini wa kujali mambo madogo – Umakini mpya ni mlango wa kurejesha ulichopoteza.

Mchakato wa Kutumia Nafasi ya Pili

Esau alipogundua ameharibu na kupoteza fursa yake:

Alikumbuka kwamba aliiuza mwenyewe miaka 20 nyuma (Mwanzo 27:36)

Alililia kwa uchungu akitafuta mbaraka wa pili (Mwanzo 27:35)

Pamoja na kwamba Esau alipoteza fursa ya kwanza, baba yake Isaka alimpa nafasi ya pili. Ingawa ilikuwa ngumu zaidi na yenye sharti gumu, bado ilikuwa fursa ya kugeuza historia yake.

Mbaraka wa Esau (Mwanzo 27:39-40)

Mbaraka huu ulihusu mambo manne:

Kuendelea kuwa mtumwa wa nduguye

Sharti kubwa katika mbaraka huu lilikuwa: “Utakuwa mtumwa wa ndugu yako, mpaka utakapoponyoka” (Mwanzo 27:40b). Esau aliamriwa kwamba angeweza kujikomboa kutoka utumwani kwa kuvunja kongwa shingoni mwake, kama ng’ombe dume anayevunja nira yake.

Kuponyoka ni ufunguo wa fursa mpya

Kuponyoka ni picha ya ng’ombe dume mwenye maamuzi ya kuvunja nira badala ya kuridhika nayo.

Mtu mmoja aliwahi kusema: “Nionyeshe mtu aliyeridhika na kiwango chake, nikuonyeshe mtu aliyefeli.”

Ili Esau aweze kufaidi fursa yake ya pili, alihitaji:

Kujipa siku na muda wa kujitambua

Kuchukua hatua za kuwajibika – “utakapoponyoka”

Kuheshimu mchakato wa mabadiliko kwa kujipa muda

Inaonekana Esau alifanikiwa katika fursa ya pili, kwani baadaye alikutana na Yakobo na hawakugombana tena (Mwanzo 33:1-16). Alikuwa amejifunza kutokana na makosa yake alipopoteza fursa ya kwanza.

Kuponyoka huleta: Kutobweteka tena, Kuwinda ndoto zako upya, Ufahamu mpya, Machaguo mapya, Fursa mpya, Tabia mpya na Matokeo mapya.

Tunaweza kugawanya maisha ya Yakobo katika sehemu nne kama za Esau na kujifunza matumizi makini ya fursa:

Sehemu ya Kwanza: Kuzaliwa na kupoteza fursa

Yakobo alipozaliwa na kugundua amepoteza fursa ya kuzaliwa wa kwanza, aliamini kuwa ana nafasi ya pili.

Sehemu ya Pili: Kununua Haki ya Mzaliwa wa Kwanza

Yakobo alipoiona fursa ya pili, alikuwa makini akaitumia kununua kitu kisichoonekana (intangible asset) –haki ya mzaliwa wa kwanza. Katika lugha ya biashara, hii ni sawa na kununua jina la biashara (brand name). Kitu cha kujifunza kutoka kwa Yakobo ni:

Imani ya kufanikiwa kwenye fursa ngumu

Sehemu ya Tatu: Uharaka wa Kuchangamkia Mbaraka

Yakobo alichangamkia kwa haraka mbaraka wa mzaliwa wa kwanza japo kwa hila. Hii inaonyesha tabia ya mtu anayejua thamani ya fursa.

Sehemu ya Nne: Kukutana na Mungu Pale Luzu

Katika Mwanzo sura ya 28, Yakobo alipoteza fursa ya kukutana na Mungu kwa kuamini akili yake, nguvu za ujana, na mipango yake mizuri. Badala ya kusubiri mwongozo wa Mungu na kurekebisha hila zake, aliondoka kwenda kupambana. Matokeo yake, alichelewesha mambo ambayo huenda angetulia na kusikiliza sauti ya Mungu angeyapata kwa njia nzuri zaidi.

Somo la Esau na Yakobo linatufundisha kwamba fursa tunazopewa na Mungu ni za thamani kubwa. Fursa zisizojirudia zinapotokea, zinahitaji umakini, busara, na hekima ya kuzitumia ipasavyo.

Fursa zote si sawa – Baadhi ni za kipekee na hazijirudii. Zitambue na zithamini.

Kupoteza fursa kuna gharama – Gharama ya kupoteza fursa ni kubwa kuliko tunavyoweza kufikiria.

Fursa ya pili inawezekana -Hata baada ya makosa, Mungu anaweza kutoa fursa nyingine, ingawa inaweza kuwa na sharti gumu zaidi.

Kuponyoka ni muhimu – Ili kufaidi fursa mpya, lazima tujikomboe kutoka katika mifumo ya zamani.

Tuwe makini na fursa unazopewa sasa – Usiwe kama Esau aliyedharau fursa yake, wala kama Yakobo aliyepoteza fursa ya kusikiliza Mungu.

Leo, Mungu anatupa fursa mbalimbali. Je, unazitambua? Je, unazithamini? Je, unazitumia kwa busara? Kama Esau, usiruhusu tamaa za muda mfupi zikuuze fursa ya maisha yako. Kama Yakobo, usiruhusu hila na akili yako zikupotezee fursa ya kusikiliza sauti ya Mungu.

Kumbuka: Fursa inapokuja, inakuja mara moja. Iitumie vizuri, kwani huenda isirudi tena.

” Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima, bali kama  watu wenye hekima, mkiukomboa wakati, kwa maana zamani hizi ni za uovu.” -Waefeso 5:15-16

Mwandishi ni Mwimbaji/Mwalimu Ambwene Mwasongwe Mwanzilishi wa Koinonia Gathering.

Kwa maombi na ushauri anapatikana 0713619931/0767619931

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports