Dodoma. Wakati mkutano wa tatu wa Bunge ukielekea ukingoni jijini Dodoma, macho na masikio ya Watanzania yanasubiri nini kitaamuliwa kwenye hitimisho la bajeti.
Hayo yanajiri baada ya mjadala wa siku saba unaohitimishwa Juni 23,2026.
Wabunge wataitwa kwa majina ili kuipigia kura bajeti ya Serikali ya 2026/27 ambayo ni Sh62.3 trilioni iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Mussa Omar Juni 11, 2026.
Bajeti hiyo ya Sh62.3 trilioni, iliyowasilishwa bungeni Juni 11, 2026 na Balozi Khamis inatarajiwa kuhitimishwa Juni 23.
Wabunge watapiga kura ya kuidhinisha au kukataa mapendekezo yaliyowasilishwa baada ya mjadala wa siku saba mfululizo.
Kabla ya hatua hiyo ya mwisho, Serikali inatarajiwa kujibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pamoja na wabunge waliochangia mjadala huo, ambao umehusisha mjadala mpana kuhusu mwelekeo wa sera za kodi na matumizi ya fedha za umma.
Miongoni mwa hoja zilizozua mjadala ni mapendekezo ya Serikali ya kuongeza ushuru wa bidhaa kwa pikipiki kwa asilimia tano pamoja na marekebisho ya ushuru kwa magari yaliyotumika kutoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, ushuru wa magari chakavu ungeongezwa kutoka asilimia 15 hadi 20.
Magari yenye miaka minane hadi 10 yangeongezwa ushuru kutoka asilimia 30 hadi 40, huku yale ya miaka 10 hadi 20 yakitozwa asilimia 50.
Kamati ya Bajeti ya Bunge imeiomba Serikali kutafakari upya mapendekezo hayo ikieleza kuwa, yanaweza kuathiri wananchi wa kipato cha chini na vijana wanaotegemea sekta ya usafiri wa bodaboda kama chanzo kikuu cha ajira.
Akizungumza bungeni wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mashimba Ndaki amesema baadhi ya mapendekezo yaliyowasilishwa yanahitaji uchambuzi wa kina zaidi ili kuhakikisha hayaleti madhara kwa makundi yakiwamo ya vijana.
Kamati hiyo pia, ilishauri Serikali kupitia upya baadhi ya marekebisho ya sheria za kodi, ikiwamo Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta pamoja na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Kwa mujibu wa kamati, baadhi ya hatua zinazotajwa katika mkakati wa kubana matumizi, zimekuwa zikirudiwa kila mwaka bila kuonekana matokeo ya moja kwa moja katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima au kuboresha ufanisi wa matumizi ya fedha za umma.
Kamati ilibainisha kuwa kuna changamoto katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, ikiwamo maandalizi hafifu yanayosababisha gharama za miradi kutokidhi thamani halisi ya fedha zinazotumika.
Kutokana na hali hiyo, ilishauri Serikali kuangalia upya bajeti ya matumizi ya kawaida na kupunguza maeneo yasiyo na athari kwa huduma za msingi ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha za umma.
Mjadala wa wabunge nao umeongeza uzito wa hoja hizo, hususan kuhusu mazingira ya ukusanyaji wa kodi na utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mbunge wa viti maalumu, Devotha Minja ameibua hoja kuhusu kile alichokiita changamoto za ukadiriaji kodi zisizoendana na uhalisia wa biashara za wananchi, akisema hali hiyo imekuwa ikiwalalamisha wafanyabiashara wengi.
Amesema baadhi ya makadirio ya kodi yamekuwa makubwa kuliko uwezo wa biashara, hali inayosababisha migogoro kati ya walipakodi na mamlaka husika.
Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe ameunga mkono hoja hiyo akisema wafanyabiashara wengi wanakumbana na mazingira magumu ya biashara yanayosababishwa na changamoto katika mifumo ya kodi na taratibu za bandari.
Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbas amesisitiza haja ya Serikali kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato ili kuzuia upotevu wa fedha na kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya kazi katika mazingira rafiki yanayochochea ukuaji wa uchumi.
Wabunge hao pia wameonya kuwa, changamoto hizo zinaweza kuathiri ustawi wa sekta binafsi iwapo hazitapatiwa ufumbuzi wa haraka, hasa kwa kuzingatia mchango wake katika ajira na mapato ya Taifa.
Wakati huohuo, Serikali inakabiliwa na jukumu la kutoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya mikopo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku baadhi ya wabunge wakieleza wasiwasi wao kuhusu mikopo kutumika kuziba nakisi ya bajeti na fedha kuelekezwa kwenye matumizi ya kawaida.
Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby ameshauri kuanzishwa kwa chombo maalumu cha kusimamia na kuchunguza matumizi ya fedha katika wizara, taasisi na miradi ya maendeleo kabla ya utoaji wa fedha zaidi, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uwajibikaji na kupunguza matumizi yasiyo na tija.
Macho yanaelekezwa kwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango, wanaotarajiwa kujibu hoja zote zilizoibuliwa kabla ya hatua ya mwisho ya upigaji kura.
Majibu yao yatabainisha iwapo Serikali itafanya marekebisho ya baadhi ya mapendekezo yaliyoibua mjadala au itaendelea na mpango wake wa awali.
Kwa wananchi, hatua hiyo itakuwa kipimo muhimu cha mwelekeo wa sera za kifedha, kodi na matumizi ya fedha za umma kwa mwaka ujao wa fedha.















