Masasi. Watu wanne wamefariki dunia baada ya gari aina ya Land Cruiser kugongana uso kwa uso na pikipiki iliyokuwa imebeba abiria, kisha kuwagonga watembea kwa miguu wawili waliokuwa pembezoni mwa barabara.
Ajali hiyo imetokea Jumamosi ya Mei 23, 2026, saa 4 usiku katika eneo la Rest Camp kwenye barabara kuu ya Masasi–Tunduru mkoani Mtwara, ikihusisha gari kuigonga pikipiki ambapo dereva aliyekuwa akiliendesha alitokomea kusikojulikana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mtaki Kurwijila, gari hilo lilihama upande wake wa kushoto wa barabara na kwenda upande wa kulia ambapo liligongana na pikipiki yenye aina ya TVS.
Kamanda Mtaki amesema pikipiki hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Stuwart Daniel (21), akiwa na abiria Noel Dastan (21), wote wakazi wa kijiji cha Nangaya, wilayani humo.
Picha ya gari ambayo imegongana uso kwa uso na pikipiki
Amesema vijana hao walifariki dunia papo hapo kutokana na ajali hiyo huku gari hilo likiendelea kupoteza mwelekeo na kuwagonga watembea kwa miguu wawili ambao majina yao bado hayajafahamika na kusababisha vifo vyao.
Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Masasi Mkomaindo kwa ajili ya taratibu nyingine.
Kaimu Kamanda huyo amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe na mwendokasi wa dereva wa gari hilo uliosababisha ashindwe kulimudu gari lake.
“Dereva alishindwa kulimudu gari lake na kuhama upande wa kushoto wa barabara kwenda kulia, hali iliyosababisha kugongana na pikipiki kabla ya kuwagonga watembea kwa miguu waliokuwa pembezoni mwa barabara,” amesema.
Amesema Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo huku juhudi za kumtafuta dereva aliyesababisha zikiendelea ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Aidha, ametoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuendesha kwa mwendo unaofaa ili kuepusha ajali zinazosababisha madhara makubwa kwa wananchi ikiwamo vifo.















