TMA yataja athari magonjwa haya msimu wa kipupwe, El-nino ikitarajiwa

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema msimu wa kipupwe unaotarajiwa kuanza Juni hadi Agosti 2026 utakuwa na hali ya baridi katika maeneo mengi ya nchi. Aidha, imesema kunatarajiwa kuambatana na upepo mkali, vumbi, magonjwa ya mfumo wa hewa pamoja na vipindi vya mvua za nje ya msimu katika baadhi ya…

admin Avatar

by

3 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema msimu wa kipupwe unaotarajiwa kuanza Juni hadi Agosti 2026 utakuwa na hali ya baridi katika maeneo mengi ya nchi.

Aidha, imesema kunatarajiwa kuambatana na upepo mkali, vumbi, magonjwa ya mfumo wa hewa pamoja na vipindi vya mvua za nje ya msimu katika baadhi ya maeneo.

Vilevile, imeeleza kuwepo kwa asilimia 90 uwezekano wa Elnino Oktoba, baada ya msimu wa Kipupwe ambao ni Juni hadi Agosti kupita.

Katika taarifa ya mwenendo wa hali ya hewa kwa kipindi cha Juni hadi Agosti, TMA imesema vipindi vya baridi kali zaidi vinatarajiwa kujitokeza Julai, huku baadhi ya maeneo yenye miinuko yakitarajiwa kushuhudia viwango vya chini vya joto vinavyoweza kushuka hadi chini ya nyuzi sita za sentigredi.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Jumatatu Mei 24, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chan’ga amesema hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo ya kanda ya ziwa Victoria, kanda ya magharibi, kanda ya kusini, nyanda za juu kusini Magharibi pamoja na Mkoa wa Singida.

Aidha, maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Pwani ya Kusini pamoja na Mkoa wa Dodoma yanatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani.

“Katika kipindi hicho, upepo wa Kusini Mashariki wenye nguvu zilizopungua kidogo kama ilivyo kawaida unatarajiwa kutawala maeneo mengi ya nchi, huku vipindi vya upepo mkali vikitarajiwa zaidi Juni na Julai katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi pamoja na maeneo ya nchi kavu,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, TMA imesema kunaweza kuwa na athari ya kuongezeka kwa magonjwa yanayohusiana na baridi ikiwamo homa ya mapafu pamoja na magonjwa ya mifugo, huku vumbi litakalosababishwa na upepo likitajwa kuongeza hatari ya maradhi ya macho, mafua na magonjwa mengine ya mfumo wa hewa.

Katika upande wa mvua, TMA imesema licha ya msimu huo kwa kawaida kuwa wa ukavu, baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupata mvua za nje ya msimu, hususan Mkoa wa Mara, maeneo ya pwani ikiwamo Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja, Pemba na Mafia.

Mvua hizo pia zinatarajiwa kujitokeza katika maeneo yenye miinuko ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.

TMA imeeleza mwenendo huo unahusishwa na kuongezeka kwa joto la bahari katika ukanda wa tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki, hali inayoashiria kujijenga kwa mfumo wa El Nino unaotarajiwa kujitokeza kuelekea Oktoba mwaka huu.

“Hali hiyo ya El Nino pamoja na ongezeko la joto katika Bahari ya Hindi upande wa Afrika Mashariki vinatarajiwa kuongeza unyevunyevu kutoka baharini kuelekea nchini, jambo litakaloweza kusababisha mvua za nje ya msimu na kupunguza ukali wa baridi wakati wa usiku katika baadhi ya maeneo,” amesema.

Amesema matarajio ya uwezekano wa Elnino Oktoba ni kwa asilimia 90, akisisitiza mamlaka hiyo itaendelea kutoa taarifa zaidi za mwenendo wake siku zijazo.

Kutokana na matarajio hayo, TMA imezitaka sekta mbalimbali kuchukua tahadhari mapema, huku wafugaji wakishauriwa kuendelea kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo na kuhifadhi malisho na maji, wakati wananchi wakitakiwa kujikinga dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na hali ya baridi na vumbi.

Pia wakulima wametakiwa kuendelea kufuata ushauri wa maafisa ugani katika maeneo yatakayopata vipindi vya mvua za nje ya msimu, huku watumiaji wa bahari wakitakiwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa kutokana na uwepo wa upepo mkali unaotarajiwa katika baadhi ya vipindi.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports