Dar es Salaam. Jumla ya watu 200 wamefariki dunia huku zaidi ya wagonjwa 850 wakihusishwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hali inayozua taharuki kubwa katika nchi jirani.
Hata hivyo, Uganda iliyokuwa na kifo kimoja cha Ebola, sasa imetoa takwimu mpya ya kuwa na wagonjwa watano, licha ya kwamba tayari imeimarisha ufuatiliaji mipakani na viwanja vya ndege ili kuzuia maambukizi kuingia nchini humo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza ugonjwa huo huenda unasambaa kwa kasi zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.
Serikali ya Uganda kupitia Wizara ya Afya imeongeza ukaguzi wa wasafiri katika maeneo ya mpakani yanayounganisha nchi hiyo na DRC, huku wahudumu wa afya wakifanya vipimo vya joto kwa wasafiri na kutoa elimu kuhusu dalili za Ebola.
Hatua hizo zinachukuliwa kutokana na historia ya Uganda kukumbwa mara kadhaa na milipuko ya ugonjwa huo unaosambazwa kupitia majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa.
Katika wakati ambao mataifa ya Afrika Mashariki yanaendelea kuwa katika tahadhari kubwa, mashirika ya misaada ya kimataifa yameonya kuwa mlipuko huo unaweka changamoto kubwa katika utoaji wa huduma za afya na misaada ya kibinadamu.
Meneja wa programu wa shirika la Médecins Sans Frontières (MSF), Kate White, amesema kuna hofu kubwa kutokana na ugumu wa kupeleka vifaa tiba na wataalamu katika maeneo yaliyoathirika nchini DRC.
White, ambaye aliondoka uwanja wa ndege wa Manchester nchini Uingereza kuelekea Congo kama sehemu ya juhudi za kimataifa za kukabiliana na Ebola, alisema mahitaji ya vifaa vya kujikinga na rasilimali nyingine ni makubwa kuliko uwezo uliopo sasa.
“Tunahitaji kuhakikisha kuwa wahudumu wote wa afya wanapata vifaa vya kujikinga kwa sababu mazingira ya sasa ni hatari sana,” alisema.
Kauli yake imekuja baada ya wafanyakazi watatu wa Shirika la Msalaba Mwekundu kufariki dunia mapema mwezi huu baada ya kuambukizwa Ebola wakati wakihusika katika shughuli za kushughulikia miili ya waliofariki.
Changamoto kubwa inayotajwa na wataalamu ni ukosefu wa chanjo rasmi dhidi ya aina ya Ebola inayosababisha mlipuko huo wa sasa. Ingawa chanjo za majaribio zinaendelea kutengenezwa, bado hakuna tiba maalumu iliyothibitishwa kutibu ugonjwa huo.
White alisema dunia imeendelea kushuhudia milipuko ya Ebola kwa miaka mingi lakini bado kuna upungufu mkubwa wa vifaa tiba, vipimo vya haraka na matibabu yanayoweza kutumika kwa ufanisi katika maeneo yenye changamoto za kiusalama.
Aidha, alieleza kuwa kufungwa kwa baadhi ya njia za anga na changamoto za usafiri vinaathiri juhudi za kupeleka misaada kwa wakati.
“Kiasi cha vifaa vinavyohitajika kwa sasa ni kikubwa mno. Tunahitaji uwezo mkubwa wa kusafirisha vifaa na wataalamu wa afya,” alisema.
Katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika, vituo vya matibabu vinaendelea kupokea wagonjwa wengi huku kukiwa na changamoto ya kuthibitisha kwa haraka kama wagonjwa wana Ebola au magonjwa mengine yenye dalili zinazofanana kama malaria.
White alisema kuna umuhimu wa kuboresha vipimo vya uchunguzi ili wagonjwa wasiokuwa na Ebola waruhusiwe mapema kurejea kwenye familia zao.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, Ebola ni ugonjwa adimu lakini hatari unaosababishwa na virusi vinavyoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Dalili zake huanza kujitokeza kati ya siku mbili hadi 21 baada ya maambukizi.
Mgonjwa huanza kupata homa kali, maumivu ya kichwa, uchovu na baadaye kutapika pamoja na kuharisha. Kadri ugonjwa unavyoendelea, unaweza kusababisha viungo vya mwili kushindwa kufanya kazi na wakati mwingine kutokwa damu ndani na nje ya mwili.
Wataalamu wanaonya kuwa ukuaji wa miji na ongezeko la watu karibu na maeneo yenye wanyama wanaobeba virusi hivyo vinaongeza hatari ya maambukizi kusambaa kwa kasi zaidi kuliko ilivyokuwa miaka iliyopita.
Kwa sasa, nchi za Afrika Mashariki zikiwemo Uganda, Rwanda, Tanzania na Kenya zinaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mlipuko huo, huku zikihimizwa kuimarisha mifumo ya afya, uchunguzi wa mipakani na utoaji wa elimu kwa wananchi ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo hatari.















