Bunda. Baadhi ya wakazi wa mji wa Bunda mkoani Mara wamelalamikia upungufu wa maji unaoukabili mji huo, hali ambayo imekuwa ikiwasababishia kero kutokana na umuhimu wa huduma wa huduma hiyo katika maisha ya kila siku.
Kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda (Buwssa) kutafuta suluhisho la kudumu juu ya changamoto hiyo ili pamoja na mambo mengine waepuke athari zitokanazo na ukosefu wa maji ikiwepo magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhara.
Wakizungumza kuhusu upungufu huo wa maji leo Mei 27, 2026, wakazi hao wamesema kumekuwepo a changamoto ya kukatika kwa maji katika mji huo, jambo ambalo limekuwa likitokea mara kwa mara, hivyo kuwa kero kwao.
“Kuna muda tunakosa maji hata kwa wiki nzima mfululizo na hili jambo sasa limekuwa ni la kawaida kabisa, na hatuoni jitihada za kumaliza kero hii tumechoka sasa tunaomba hatua zichukuliwe,” amesema Anifa Ibrahim.
Amesema inashangaza kuona mji huo ukikabiliwa na changamoto hiyo licha ya kuwepo kwa mradi mkubwa wa maji wa Nyabehu ambao tayari umeanza kutoa huduma na kusema uwepo wa mradi huo kunatakiwa kwenda sambamba na upatikanaji wa uhakika wa maji kwa wakazi hao.
“Kwa sasa imekuwa kawaida kukosa maji kwa zaidi ya siku tatu na hii tabia imeanza kushamiri ma kuota mizizi, wakati huo tunaona kuna miradi kadhaa imetekelezwa sasa tunajiuliza, tija ya hii miradi iko wapi?” amehoji Hilda Masubo.
Ameomba mamlaka husika kushughulikia suala hilo kwa haraka ili wananchi waondokane na kero hiyo ambayo amesema, pia, inachangia kurudisha nyuma jitihada za wananchi katika kushiriki kwenye shughuli za maendeleo kwaajili ya kuinua kipato na uchumi wao kwa ujumla.
Akizungumza suala hilo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Bunda, Ester Gilyoma amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema inasababishwa na kupasuka kwa bomba kuu.
Gilyoma amefafanua kuwa bomba hilo linalosafirisha maji kutoka kwenye chanzo cha maji Nyabehu kuja mjini limekuwa likipasuka mara kwa mara kutokana na kushindwa kuhimili msukumo mkubwa wa maji.
Ameongeza kuwa kwasasa wanatekeleza mradi wa kujenga bomba jipya litakalokabiliana na changamoto hiyo mradi ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 50.
“Ni kweli mradi wa maji Nyabehu ulishaanza kutoa huduma na hadi sasa usambazaji wa maji safi na salama mjini Bunda ni asilimia 87 lakini tumepata changamoto ya bomba kuu kushindwa kuhimili ‘pressure’ ya maji na tayari jambo hili linafanyiwa kazi muda si mrefu tutamaliza kabisa changamoto hii,” amesema
Amewataka wakazi hao kuwa wavumilivu katika kipindi hili ambacho maboresho yanafanyika ili kupata suluhu ya kudumu ya changamoto hii.
Amesema dhamira ya Serikali ya kuboresha upatikanaji wa maji bado iko pale pale na ndio maana kuna utekelezaji wa miradi kadhaa ya maji mjini humo ili kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa asilimia 100.















