Kesi ya mgogoro wa rasilimali Chadema ilivyoanza hadi kutupwa

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshinda kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali usio sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar inayokikabili. Chama hicho kimeshinda kesi hiyo baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kuitupilia mbali kabla ya kuisikiliza madai ya msingi kufuatia pingamizi la awali ambalo kililiibua kuhusiana…

admin Avatar

by

5 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshinda kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali usio sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar inayokikabili.

Chama hicho kimeshinda kesi hiyo baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kuitupilia mbali kabla ya kuisikiliza madai ya msingi kufuatia pingamizi la awali ambalo kililiibua kuhusiana na uhalali wake.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji David Ngunyale leo Alhamisi, Mei 28, 2026 imekubaliana na hoja za pingamizi la Chadema kuwa kesi hiyo si halali kwa kuwa hati ya madai ina kasoro za kisheria kutokana na kutokubainisha kuwa mambo yaliyokuwa yanalalamikiwa na wadai yalianza lini.

“Katika mazingira hayo, Mahakama hii inaona kuwa hati ya madai ina kasoro za kisheria na hivyo inaitupilia mbali,” amesema Jaji Ngunyale akihitimisha uamuzi huo na kuelekeza kila upande ubebe gharama zake za uendeshaji kesi hiyo.

‎Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilifunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

‎Wadaiwa katika kesi hiyo walikuwa ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Katika kesi hiyo wadai walikuwa wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

‎Pia, walikuwa wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo pamoja na mambo mengine walikuwa wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.

Awali, wadaiwa waliibua pingamizi la awali wakiiomba mahakama hiyo iitupilie mbali pamoja na hoja nyingine wakidai imefunguliwa nje ya muda uliowekwa na Sheria ya Ukomo wa muda, inayotaka kesi kama hiyo ifunguliwe ndani ya miaka sita tangu kutokea kwa sababu ya madai husika.

Hata hivyo, Mahakama Kuu pamoja na kuamua hoja nyingine za pingamizi hilo ambazo ilizikataa, haikuitolea uamuzi hoja hiyo ya kufunguliwa nje ya muda.

Badala yake iliendelea na hatua nyingine za usikilizwaji wa kesi hiyo ya msingi pamoja na mashauri mengine madogo yaliyotokana nayo.

Baadaye Mahakama ya Rufani kwa maelekezo ya Jaji Mkuu ilifanya mapitio ya kesi hiyo na mashauri madogo yaliyofuatia.

Katika uamuzi wake ilioutoa Aprili 15, 2026, Mahakama ya Rufani ilibatilisha sehemu ya mwenendo wa uamuzi wa Mahakama Kuu uliokizuia chama hicho kwa muda kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo itakapomalizika.

Pia Mahakama hiyo ilielekeza kesi hiyo isikilizwe na jaji mwingine tofauti na Jaji Hamidu Mwanga aliyekuwa akiisikiliza awali pia ikaelekeza jaji huyo mpya aanza kusikiliza pingamizi la Chadema kuhusiana na ukomo wa muda.

Hivyo kesi hiyo ilipangwa kwa Jaji Ngunyale ambaye Mei 20, 2026 alisikiliza pingamizi hilo kama Mahakama ya Rufani ilivyoelekeza.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa wadaiwa (watoa pingamizi) Mpale Mpoki alieleza  mahakama kuwa kesi haipaswi kuwepo mahakamani kwa kuwa waombaji hawakukidhi matakwa ya Amri ya VII kanuni ya 1(e) ya Kanuni za Mwenendo wa Mashauri ya Madai (CPC).

Alidai kuwakatika hati ya madai hakuna hata aya moja inayozungumzia kuwa ni lini sababu ya madai ilitokea na kwamba katika aya ya nne ya hati ya madai waombaji wanaeleza kuwa sababu za madai yao bila kueleza zilianza lini.

Wakili Mpoki kwa niaba ya mawakili wenzake, Dk Rugemeleza Nshala, Hekima Mwasipu na Selemani Matauka, alidai kuwa madhumuni ya matakwa ya kanuni ya 1(e) ni kuiwezesha mahakama kutambua kama kesi imefunguliwa ndani ya muda au la.

Huku akiirejesha mahakama katika uamuzi wa kesi mbalimbali zilizokwishakuamuliwa na Mahakama Kuu na zingine Mahakama ya Rufani, wakili Mpoki alidai kuwa kesi nyingine zimekuwa zikiondolewa mahakamani kwa kutokukidhi matakwa ya kanuni hiyo.

Akijibu hoja hiyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai (wajibu pingamizi), Shabani Marijani alidai kuwa hati ya madai ya kesi hiyo imeonesha ni lini sababu za madai zilianza.

Aliielekeza mahakama katika aya ya saba mpaka ya 16 ambazo alidai nyingine zimetaja tarehe, mwezi na mwaka na nyingine zikionesha kuwa mambo wanayoyalalamikia yanaendelea mpaka sasa.

Wakili Marijani, akisaidiwa na mawakili Gido Simfukwe na Alvan Fidelis, alisisitiza kuwa kwa sababu hizo kesi hiyo imefunguliwa ndani ya muda wa ukomo kama inavyotakiwa kisheria.

Alisema suala hilo litahitaji ushahidi zaidi jambo ambalo linafanya pingamizi hilo likose sifa za kuwa pingamizi la awali.

Hata hivyo, wakili Dk Nshala alieleza aya ya saba mpaka ya 14 ya hati ya madai zilizorejewa na mawakili wa wadai hazielezi ni lini mgogoro ulianza na kwamba zinaeleza tu mambo wanayoyalalamikia.

“Kwa mfano aya ya 20 haisemi kuwa tarehe fulani mahali fulani viongozi fulani walisema maneno ya kuvunja Muungano,” alisisitiza Dk Nshala na kuhitimisha;

“Kwa hiyo kutokana na kasoro kubwa zilizomo katika kesi hii mahakama yako inakuwa haina mamlaka ya kuisikiliza na kwamba ina kasoro zisizorekebishika na inatakiwa kufukuzwa.”

Kabla ya kuamuliwa kwa pingamizi hilo mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu alifungua shauri dogo la maombi akiomba kuunganishwa katika kesi hiyo kama mdaawa muhimu akidai kuwa ana masilahi makubwa katika kesi hiyo, ambalo lilipangwa kusikilizwa Juni 2, 2026.

Jaji Ngunyale baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake jana, Alhamisi Mei 29, 2026 alisema kuwa Mahakama imeridhika kuwa pingamizi hilo liko sahihi kisheria.

Alisema kuwa baada ya kupitia vizuri hati ya imetaja mwaka 2019 na 2014 kwa ujumla kwa baadhi ya matukio.

Alisema Amri ya VII kanuni ya 1(e) ya CPC inataka kubainisha muda rasmi ambao madai ya ukiukwaji unaolalamikiwa ulianza.

Hata hivyo amesema kuwa baada ya kupitia kwa kina imeona hakuna tarehe rasmi inayoeleza kuwa mgogoro huo ulianza lini.

“Hivyo mahakama inashindwa kujiridhisha kama ina mamlaka kuisikiliza kesi hii au la. Kitendo cha mahakama kushindwa kuona mgogoro ulianza lini ni upungufu ambao mahakama inayosimamia sheria haiwezi kuuacha hivihivi,” amesema Jaji Ngunyale.

Kwa uamuzi huo hata shauri la maombi la Lissu lililopangwa kusikilizwa Juni 2, 2026 limekufa kifo cha kawaida kwani uhai wake ulitegemea kuwepo kwa kesi hiyo ya msingi.

Akizungumzia uamuzi huo, wakili Marijani amesema kwa aina ya uamuzi huo bado wana nafasi ya kufungua upya kesi hiyo baada ya kufanya marekebisho ya kasoro ambayo Mahakama imeibainisha.

“Hivyo tunakwenda kushauriana na wateja wetu, kama wakiridhia basi tutaifungua upya,” amesema wakili Marijani.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports