Tanzania, Italia kukuza ajira vijana Ruvuma

Songea. Ushirikiano kati ya Tanzania na Italia umetajwa kuwa mkakati muhimu wa kukuza fursa za kiuchumi, ajira na ujuzi kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu nchini. Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, wakati akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa Jenga Uwezo na Ajira (JUA) unaotekelezwa na Shirika…

admin Avatar

by

2 minutes

Read Time

Songea. Ushirikiano kati ya Tanzania na Italia umetajwa kuwa mkakati muhimu wa kukuza fursa za kiuchumi, ajira na ujuzi kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu nchini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, wakati akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa Jenga Uwezo na Ajira (JUA) unaotekelezwa na Shirika la Cooperative Paesi Emergenti (COPE), uliofanyika katika uwanja wa Veta Manispaa ya Songea.

RC Ahmed amewataka vijana mkoani Ruvuma kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa zilizopo katika kilimo, ufugaji na ufundi stadi ili waweze kujikwamua kiuchumi na kupunguza umasikini.

Amesema Italia imeonesha nia ya kusaidia nchi mbalimbali za Afrika kupitia miradi ya maendeleo inayolenga kubadilishana uzoefu, ujuzi na maarifa katika sekta tofauti, hivyo vijana wanapaswa kutumia fursa hizo kikamilifu.

RC Ahmed amesisitiza kuwa pamoja na fursa zinazotolewa, bado mwitikio wa vijana katika mafunzo ya kilimo, ufugaji na ufundi ni mdogo, hivyo amewataka kubadilika na kuwa na mwamko wa kushiriki shughuli za uzalishaji.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kimataifa, Ali Mussa Balozi, amesema ushirikiano huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya diplomasia ya uchumi inayolenga kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa makundi mbalimbali nchini.

Amesema Tanzania na Italia zinashirikiana kwa vitendo katika kuwainua vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia miradi inayolenga kukuza ujuzi na fursa za ajira.

Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Sean Coppola, amesema mradi wa JUA unawalenga vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika maeneo ya Manispaa ya Songea, Songea Vijijini na Wilaya ya Namtumbo.

Amesema lengo kuu la mradi huo ni kukuza uchumi endelevu na jumuishi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa ajira zenye tija na kazi za staha kwa wote, sambamba na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 8) ya Umoja wa Mataifa.

Coppola ameongeza kuwa mradi huo pia unalenga kuboresha sera zinazosaidia uzalishaji, ujasiriamali, ubunifu na ukuaji wa biashara ndogo na za kati katika maeneo yanayotekelezwa mradi.

Naye Meneja wa Mradi wa JUA, Eleonora Bolliger, amesema Italia inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini Tanzania, hususan katika mnyororo wa thamani wa kahawa.

Amesema mradi huo unalenga kuongeza ujuzi wa kiufundi na ujasiriamali kwa wakulima vijana na wanawake ili kuboresha uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao.

Bolliger ameeleza kuwa ushirikiano huo unaonyesha namna wadau wa maendeleo, Serikali za mikoa na asasi za kiraia wanavyoweza kufanya kazi kwa pamoja, na akatumaini kuwa sekta binafsi ya Italia itaendelea kuwekeza zaidi katika fursa zilizopo mkoani Ruvuma.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports